Madiwani Butiama kuubana mgodi mahakamani

MADIWANI wa Kata za Kyanyari, Kamugegi na Kukirango zinazopakana na Mgodi wa Dhahabu wa Cata Mine,Wilaya ya Butiama mkoani Mara, wanakusudia kufungua kesi mahakamani dhidi ya mgodi huo kwa kutolipa Fedha za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).

Hayo yameelezwa na Ofisa Maliasili na Uhifadhi wa Mazingira wa halmashauri hiyo, Lowitu Loishiye, aliyemwakilisha Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Patricia Kabaka kwenye ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mzee kwenye mgodi huo.

Huo ni mgodi wa Sita kutembelewa na kiongozi huyo katika Wilaya za Tarime na Butiama, amesema hakufurahishwa na  hali aliyoshuhudia ya wawekezaji kuvuna utajiri, katikati ya umaskini uliyokidhiri.

“Kuelekea migodini Tarime hakuna barabara nzuri, Buhemba hata wachimbaji wanaishi kwenye vihema na vibanda vya bati, hapa (CATA Mine) ukisoma nyaraka zinafurahisha, lakini kwenye uhalisia hakuna kitu,” anasema Meja Jenerali Mzee.

Amesema kupitia ziara hiyo, mpaka wakati akizungumza alikuwa amejiridhisha uwepo wa shida mahala, kwa upande wa migodi au kwa wenye dhamana ya kusimamia utekelezaji wa sheria katika migodi, hususani eneo la uwajibikaji kwa jamii.

Alihoji mpango wa mgodi huo kujenga vyumba vitatu katika Zahanati ya Nyakisiwa, ikiwa sehemu ya CSR na kuelezwa na Mwanasheria wa Kampuni hiyo, John John kwamba ilitakiwa kutoa Sh milioni 17 kwa utaratibu wa kutanguliza Sh milioni 5.

Hata hivyo, ilielezwa na Loishiye kuwa CSR hiyo ilitakiwa kulipwa mwaka wa fedha uliyoishia Juni 31, 2021 na hivyo kuanzia Julai Mosi, mwaka huu, kisheria wanatakiwa kuwa na miradi mingine inayotakiwa kutekelezwa ndani ya mwaka utakaoishia Juni 31, 2023.

“Wenzetu wamekuwa wagumu kulipa CSR mpaka madiwani wa kata zinazozunguka mgodi wameleta hoja ya kutaka kuupeleka mahakamani, bado tunalishughulikia hili,” anasema Loishiye.

Mkuu huyo wa Mkoa  ametoa siku saba kwa mgodi huo kulipa fedha yote hiyo Sh milioni 17 kwa ajili ya CSR ya mwaka jana na kutekeleza taratibu za kisheria kwa ajili ya kulipa CSR ya mwaka huu.

 

Habari Zifananazo

Back to top button