IRINGA; BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, limetoa onyo lingine kwa watendaji wanaoisababishia hoja za ukaguzi halmashauri hiyo, likisema litaendelea kuchukua hatua kali dhidi yao, ikiwemo kuwafikisha katika vyombo vya dola na hata kuwafukuza kazi.
Azimio hilo limetolewa na baraza hilo katika mkutano wao maalumu uliokuwa ukijadili hoja za ukaguzi wa nje zilizotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2022/2023.
Akifungua mkutano huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa Peter Serukamba, Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa, Doris Kalasa amesema katika mwaka huo wa fedha CAG alifanya ukaguzi katika halmashauri hiyo na jumla ya mapendekezo 25 ya taarifa kuu yalitolewa.
Kati ya mapendekezo hayo, alisema tisa ni ya sasa na 16 ni ya miaka ya nyuma, huku kukiwa na mapendekeo mengine matano yanayohusu miradi ya mfuko wa afya na sita yanayohusu mfuko wa wanawake, vijana na watu wenye ulemevu.
“Naagiza chukueni hatua za kisheria kwa wale wote wanaoisababishia au kuiingiza halmashauri yenu katika hoja za ukaguzi zisizo na msingi,” amesema.
Ametaja baadhi ya hoja zilizoibuliwa na CAG katika ukaguzi huo kuwa ni pamoja na Sh Milioni 200 za wadaiwa katika mfumo wa kukusanya mapato (LGRCIS), Sh Milioni 45.9 zilizokusanywa bila kuwekwa benki, na Sh Milioni 52.2 zilizochukuliwa zaidi katika mfuko wa amana.
Zingine ni pamoja na utendaji usioridhisha wa mfumo mpya wa ukusanyaji mapato (TAUSI), kuchelewa kukamilika kwa miradi ya maendeleo ya thamani ya Sh Milioni 842.1, madai ya Sh Bilioni 3.1 ambayo hayakujumuishwa kwenye makadirio ya mwaka na Sh Milioni 134.4 za mapato ya ndani ambazo hazijatengwa kwa shughuli za maendeleo.
Zingine ni ununzi wa dawa na vifaa tiba vya Sh Milioni 40.3 kwa wauzaji binafsi bila kuwa na hati kutoka Bohari ya Dawa (MSD), taarifa zisizo sahihi za shughuli zilizotekelezwa kwa Sh Milioni 44.3 na ripoti pungufu ya mali ya kiasi cha Sh Milioni 293.1 katika mfuko wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu na mikopo ambayo haijarejeshwa ya zaidi ya Sh Milioni 375.
Akitangaza majibu ya menejimenti katika mkutano huo, Mkuu wa Kitengo cha Fedha na Uhasibu, Jwani Yengi amesema menejimenti imezingatia maoni yote ya mkaguzi na baadhi yamekwishafanyiwa kazi huku mengine yakiendelea kushughulikiwa.
Akitoa mfano wa fedha kiasi cha Sh Milioni 45.9 zilizokusanywa bila kupelekwa benki alisema kiasi cha sh 1,374,340 kilikusanywa na kupelekwa benki na hatua ikiwemo ya mtumishi mmoja kufukuzwa kazi, mmoja kufikishwa Polisi huku wengi uchunguzi wao ukiendelea kufanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Wakati baraza hilo likiweka azimio la kuchukua hatua kali kwa watumishi watakaoendelea kuisababishia hoja halmashauri hiyo, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Steven Mhapa alisema; “Hatutakubali kuzalisha hoja mpya. Baada ya kupitia ripoti hii ya CAG tunajipanga kuzimaliza hoja zote na tunatambua kazi iliyotuleta madiwani ni kusimamia mapato na matumizi ya halmashauri.”