BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Iringa kwa kauli moja limeazmia kuwafuta kazi watumishi watatu na wengine wawili kukatwa asilimia 15 ya mishahara yao kwa miaka mitatu mfululizo waituhumiwa makosa mbalimbali ikiwemo wizi wa fedha, utoro kazini na ulevi, na kuisababishia halmashauri hasara.
Azimio hilo la pamoja limetolewa katika kikao cha baraza hilo katika ukumbi wa ofisi mpya za halmashauri hiyo zilizopo Ihemi kilometa 35 kutoka mjini Iringa.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Steven Mhapa amesema wamefanya maamuzi hayo baada ya kujiridhisha na maelezo yaliyotolewa kwa pande zote, hivyo adhabu hizo ni kwa mujibu wa kanuni za kiutumishi.
Watumishi walio angukia adhabu ya kufukuzwa kazi ni pamoja na Abel Ndelingo aliyekuwa fundi sanifu wa shule ya sekondari ya wasichana Ifunda kwa kosa la kutokuwepo kituo cha kazi kwa zaidi ya mwaka bila taarifa.
Wengine ni Abdulatifu Issa aliyekuwa Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Mambao anayetuhumiwa ubadhirifu wa fedha ya halmashauri zaidi ya Sh Milioni 1.8 na Olivo Utenga aliyekuwa mtendaji Kijiji cha Makuka anayetuhumiwa kuchukua vitabu vya stakabadhi za malipo na upotevu wa fedha zilizokusanywa.
Mhapa aliwataja watumishi wawili walioangukia adhabu ya kukatwa mshahara kuwa ni Watson Kafumbwe fundi sanifu daraja la kwanza wa shule ya sekondari Tosamaganga aliyehusishwa wizi wa kemikali za maabara na mwingine ni Johaveni Mujuni muuguzi wa Zahanati ya Tungamalenga kwa kosa la Ulevi.
Watumishi wote waliopewa adhabu hii hawakuwepo katika kikao hicho na Mhapa akatumia nafasi hiyo kuwaonya watumishi wote wanaofanya kazi kwa mazoea kuacha mara moja, akisema halmashauri yake haitamvumilia mtumishi mzembe na asiyejali maslahi ya umma.