Madiwani waomba kibali cha kuvuna mamba

BARAZA la Madiwani katika Halmashauri ya Nsimbo Mkoa wa Katavi, wameiomba Wizara ya Maliasili na Utalii kuja na mpango maalumu wa kuvuna mamba kwenye Mto Ugalla kwani wamekuwa wakisabisha vifo kwa wananchi.

Diwani wa Kata ya Mtapenda, Elieza Fyula ameibua hoja hiyo wakati akichangia hoja za kamati kwenye baraza hilo na kueleza kuwa kipindi cha nyuma waliomba ushauri huo wa kuwavuna mamba hao kwenye Mto Ugalla na hali ikawa nzuri.

“Huko nyuma mamba waliua watu wengi sana Ugalla na tulishauri ipelekwe kampuni na kupewa zabuni kwa ajili ya kuwinda wale wanyama wakapungua na maisha ya watu yakasalimika, sasa hii hali imejirudia labda mamba wamezaana sana,” amesema Fyula na kuongeza kuwa ni vyema hatua za haraka zikachukuliwa ili wananchi wawe salama.

Naye Diwani wa Kata ya Nsimbo, Michael Kasanga amesema hali hiyo inatokana na wananchi hususani wa maeneo ya vijiji vya Katambike kutegemea maji ya Mto Ugalla kwenye shughuli zao za kila siku, wakiwa huko hupatwa na madhila ya kutafunwa na mamba.

“Chanzo cha kuliwa wananchi na mamba ni pamoja na uhaba wa maji, wanaenda kufuata maji kwenye sehemu ambayo mamba wapo na mamba wanakaa pale kwa kuwasubiri,” amesema Kasanga .

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Nsimbo Charles Halawa, ambae pia ni Diwani wa Kata ya Ugalla amesema tatizo hilo kwenye Kata ya Ugalla lipo na watahakikisha hatua za maksudi zinachukuliwa, ili kumaliza kero hiyo.

“Hao wanachi wanaozungumzwa wapo kwenye kata yangu, juzi tumempoteza mtoto aitwae Mrisho Msombola mwenye miaka 14 alikuwa mwanafunzi wa Darasa la Saba, ameuawa na mamba kwa hiyo linapozungumziwa suala la mamba tuwe serious kidogo,” amesema Halawa.

Akijibu hoja hiyo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nsimbo ,Mohamed Ramadhan amesema tayari wameshaandika barua kwenda Wizara ya Maliasili na Utalii kwa ajili ya kuomba kibali cha uvunaji wa mamba hao.

“Tulifanya jukumu la kuandika barua Wizara ya Maliasili kwa ajili ya kuomba kibali cha kuvuna mamba na mpaka sasa bado hatujapokea majibu yeyote ya kukubaliwa kibali hicho au la,” amesema Ramadhan.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x