Madiwani washangazwa mradi wa shule kukwama Geita

MADIWANI wa Halmashauri ya Mji wa Geita mkoani Geita wamelalamikia na kushangazwa na kukwama bila taarifa kwa mradi wa ujenzi wa shule ya mchepuo wa kiingereza uliopitishwa miaka mitatu iliyopita.
Mradi wa shule hiyo ya msingi ulipangwa kujengwa kwa majengo ya ghorofa moja katika kata ya Bombambili mjini Geita kupitia fedha za Uwajibikaji wa Makampuni kwa Jamii (CSR) kutoka GGML.
Hoja hiyo imeibuliwa na diwani wa kata ya Bombambili, Leonard Bugomola katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Mji na kuhoji kwa nini mradi haujaanza ingali hatua zote zipo tayari.
“Wakati tunaianzisha hii shule ya ‘English Medium’ ilileta kelele. Tukatafuta eneo jingine ambalo ni dogo  tukasema tuanzishe kwa ujenzi wa ghorofa.
“Mpaka sasa hivi tunavyoongea changamoto siyo upande wa CSR, wenzetu kule GGML wapo tayari wanasubiri michoro kutoka halmashauri toka mwaka jana.”
Bugomola amehoji inakuwaje halmashauri ilikuwa tayari imetoa ramani ya mchoro wa ujenzi lakini mara baada ya GGML kutaka kusimamia kila kitu katika ujenzi huo taarifa zikatoka hakuna ramani.
Diwani wa kata ya Nyanguku, Elius Ngole amesema kikwazo kikubwa kinaonekana kuwa ni watalaamu wa halmashauri ambao wameshindwa kutoa mchoro wa shule hiyo kwa mfadhili ambaye ni GGML.
Diwani wa kata ya Buhalahala, Dotto Zanzui amesema tatizo ni wahandishi wa halmashauri kwani ndio wameonekana kukwamisha miradi mingi ya CSR ndani ya halmashauri hiyo.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Geita, Mussa Mbyana amesema ili kupata ufumbuzi yakinifu wa changamoto ya mradi huo ni vyema kusubiri majawabu ya kikao maalum cha kujadili miradi ya CSR.
“Kama inshu ni ramani sidhani kama siku zote wanakutana GGML na  wataalamu wa halmashauri washindwe kuijua inshu ya ramani.”  Ameeleza.
Makamu Mwenyekiti wa Halamashauri ya mji wa Geita, Prudence Temba ameelekeza halmashauri iandae haraka kikao cha kujadili masuala ya CSR ili kupata hatima kamili ya mradi wa shule hiyo.
“Kwa sababu kila tukigusa CSR inaonekana kuna shida kila mahali, sasa tupate watalaamu, tushirkiane na atu wa GGML, mkurugenzi awepo na watu wengine ili tuweze kupata majibu ya uhakika.”

 

Habari Zifananazo

Back to top button