Madiwani wataka gharama za wajawazito ziwekwe wazi

KAGERA; Meya Manispaa ya Bukoba, Gibson Godson ameitaka Idara ya Afya Manispaa ya Bukoba kuhakikisha wanaweka wazi gharama za vipimo, dawa, vifaa vya kujifungulia na huduma zote kwa mama wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano katika mbao za matangazo kwa vituo vyote vya afya na zahanati  vinavyopatikana katika manispaa hiyo.

Godson ametoa agizo hilo ikiwa ni makubaliano ya Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Bukoba, baada ya kuibuka hoja  kwenye kikao cha robo ya kwanza mwaka wa Fedha 2023/2024 kutoka kwa Diwani wa Viti maalumu, Kata ya Kashai, ambaye pia ni Naibu Meya Mwajabu Galiatano.

Diwani huyo alitaka kujua sababu za wanawake kutozwa gharama mbalimbali wakati wa ujauzito, mahudhurio ya kiliniki pamoja na kununa dawa kabla au baada ya kujifungua, wakati sera na maagizo ya Wizara ya Afya yamekuwa yakisema huduma hizo ni bure.

Amesema kwa muda mrefu wanawake wamekuwa wakipishana nyumbani kwake na ofisini wakiomba  kupunguziwa gharama za kununua vifaa vya kujifungua, vipimo huku wengine wakiogopa rufani za kwenda kujifungulia hospitali nyingine kwa kuhofia gharama kuongezeka.

Amesema sio yeye peke yake bali madiwani wengi wamekuwa wakipokea malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu suala la gharama hizo.

” Sasa baraza hili la madiwani tuwekwe wazi, kwamba ni kitu gani kinapaswa kulipiwa , wachapishe waweke katika ubao, lakini pia jukumu la kuwaelimisha toka wanavyoanza kiliniki lifanywe na wataalamu wetu wa afya ,bado watoto wakizaliwa dawa zinanunuliwa jambo hilo linashangaza,”amesema Galiatano.

Hoja hiyo iliibua mjadala kutoka kwa madiwani wengine, ambapo baadaye Meya alisema kuna haja ya kubainisha gharama zote za wajawazito na watoto ziwekwe kwenye mbao za matangazo ili kuondoa uchonganishi kati ya wananchi na serikali yao.

Akizungumzia suala hilo, Kaimu mganga mkuu Manispaa ya Bukoba,  Ausoni Baruti amesema vifaa vinavyolazimika kununuliwa katika maduka ya dawa ya hospitali kwa wanaojifungua na hata watoto wachanga ni zile ambazo hazipo kwa muda huo.

Hata hivyo amesema bado vituo vyote vya vya kutolea huduma vinatoa fursa kwa kila mtu ambaye hana msaada au uwezo kwa kupata vifaa hivyo bure bila gharama yoyote.

Habari Zifananazo

Back to top button