KIGOMA: Madiwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma wameiomba serikali kulikabidhi jeshi la polisi kazi ya kupambana na vitendo vya waganga matapeli maarufu kama Kamchape kutokana na vitendo vya waganga hao kuleta athari kubwa kwa jamii.
Madiwani hao wametoa kauli hiyo katika kikao cha robo ya pili cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/2024, ambapo wamependekeza kuwa kwa hali ya sasa ni vizuri jeshi la wananchi likaongezwa kwenye kazi hiyo ili kusaidiana na jeshi la polisi ambao kwa muda mrefu ndiyo waliokuwa wakisimamia kupambana na waganga hao.
Pendekezo hilo la madiwani linakuja baada ya hoja ya diwani wa Kata ya Bugaga, Hitla Joseph kutoa hoja ya dharura kuhusu suala hilo la ‘kamchape’ ili lijadiliwe huku akieleza madhara yaliyosababishwa na kamchape au kwa jina lingine ‘lamba lamba’.
Diwani huyo akizungumza huku akitoa mifano alisema kuwa kata ya Kurugongo mchungaji alipigwa na wananchi waliofuatana na waganga hao matapeli na mali zake kuharibiwa kwa madai ya kuwa ni mchawi ambapo pia katika kata hiyo mama mmoja alimwagiwa maji ya moto kwamba ni mchawi hiyo kuathirika kimwili na kiakili.