Madrid, City usiku wa kisasi

USIKU wa mabingwa unarejea leo, ambapo kutapigwa mchezo wa kwanza wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kati ya Real Madrid ambao watakuwa nyumbani Santiago Bernabeu wakiwakaribisha Machester City.

Itakuwa mechi ya kisasi ya nusu fainali ya mwaka jana wakati Madrid ilipoiondoa City mabao 6-5 na kushinda taji la 14 Ulaya.

Man City ilishinda mabao 4-3 katika mchezo wa kwanza uliopigwa April 2022, na Real Madrid kushinda mchezo wa pili mabao 3-1 mchezo uliopigwa Mei 2022, hivyo Madrid kwenda Fainali kwa mabao 6-5.

Haaland mwenye umri wa miaka 22 amefunga mabao 12 kati ya 26 ya City kwenye Ligi ya Mabingwa msimu huu. Anahitaji mabao matano zaidi kufikia rekodi ya Cristiano Ronaldo ya msimu mmoja ya mabao 17 akiwa na Madrid msimu wa 2013-14.

Manchester City, inayoonekana kutozuilika inasaka kuwa timu ya pili ya Uingereza kushinda mataji matatu ya Ligi ya Mabingwa, EPL na Kombe la FA baada ya wapinzani wao Manchester United kufanya hivyo mwaka wa 1999.

Real Madrid, inayoshika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa La Liga na ikiwa nyuma ya vinara Barcelona kwa pointi 14, wataingia wakiwa na hali ya kujiamini baada ya kutwaa Kombe la Mfalme Jumamosi kwa mara ya kwanza tangu 2014.

Madrid wana historia ya kuzifunga timu za Uingereza. Msimu huu wamezitupa nje Liverpool na Chelsea huku mwaka jana wakizifunga Chelsea, City na Liverpool na kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Beki wa kati wa Real Madrid, Militao amefungiwa kucheza mechi moja baada ya kupata kadi tatu za michuano hiyo katika ushindi wa robo fainali ya pili dhidi ya Chelsea.

Beki wa kushoto Ferland Mendy atakosa mchezo huo kutokana na tatizo la kifundo cha nyuma ya mguu.

Kiungo wa Madrid, Luka Modric, 37, anatarajiwa kukichezea kikosi cha Carlo Ancelotti baada ya kupona jeraha la misuli ya paja.

Beki wa City, Nathan Ake huenda akakosa kucheza baada ya kupata jeraha wakati wa ushindi wa 2-1 dhidi ya Leeds United Jumamosi.

Pep Guardiola anatarajiwa kuwakaribisha wachezaji wa kawaida wa City Jake Grealish, John Stones, Rodri na Bernado Silva, ambao walipumzishwa dhidi ya Leeds.

Kevin De Bruyne wa City alirejea kutoka kwa jeraha kwa mchezo huo na kuna uwezekano wa kuanza leo.

Habari Zifananazo

Back to top button