Maelfu ya vyeti vya kughushi maombi Bodi ya Mikopo
WAKALA wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) umebaini vyeti 6,981 vya kuzaliwa na vifo vina upungufu ikiwamo kughushi kati ya 127,292 vilivyowasilishwa kuhakiki uhalali wa waombaji mikopo ya elimu ya juu.
Rita jana ilitoa taarifa iliyoeleza kuwa kuanzia Juni Mosi, mwaka huu ilipokea maombi ya kuhakiki vyeti 135,184 vikiwamo 116,867 vya kuzaliwa na 18,317 vya vifo.
Utaratibu wa kuomba mkopo katika Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) unaelekeza waombaji waambatanishe nakala ya cheti cha kuzaliwa kilichohakikiwa na Msajili Mkuu wa Vizazi.
Utaratibu huu pia unaelekeza waombaji waambatanishe cheti au vyeti vya vifo vya wazazi.
Rita imeeleza kuwa lengo la kuhakiki ni kuhakikisha kila anayeomba na kupata mkopo wa masomo unaotolewa na serikali ni anayestahili kutokana na vigezo vilivyowekwa.
“Kufikia Jumanne wiki hii wakala umeshahakiki maombi 127,292, sawa na asilimia 94, ambapo maombi 6,981 yalionekana kuwa na mapungufu,” alisema Ofisa Mtendaji Mkuu wa Rita, Angela Anatory jana kwenye taarifa iliyosambazwa kwenye vyombo vya habari.
Alieleza kuwa baadhi ya upungufu katika maombi hayo ni vyeti vya kughushi au havionekani katika kumbukumbu za Msajili Mkuu.
Upungufu mwingine ni nakala zisizosomeka au namba ya ingizo kutoonekana au kutuma nakala ya vyeti vilivyotolewa nje ya nchi ambavyo Rita haina mamlaka ya kuvihakiki.
“Wakala umeimarisha kitengo kinachoshughulikia maombi ya uhakiki kuhakikisha maombi yanajibwa mara tu yanapopokelewa ili kuwawezesha waombaji waweze kuendelea na taratibu nyingine za kuomba mikopo ya elimu,” alisema Anatory.
Aliongeza: “Natoa rai kwa wananchi wote kufuata taratibu na mifumo sahihi ya kutuma maombi ya huduma zetu ili kuepuka kuingia mikononi mwa vishoka ambao huwapatia nyaraka zisizo halali hivyo kuwasababishia usumbufu.”
Alieleza kuwa Rita inaendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha wananchi wasio waaminifu (vishoka) wanabainika na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Alisema ili kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma, Rita inaendelea kuboresha mifumo ya tehama kuwawezesha wananchi kupata huduma pale walipo hivyo kuwawezesha wananchi wengi zaidi kupata huduma kwa gharama nafuu.
Rita ni wakala wa serikali wenye jukumu la kusimamia na kuratibu usajili wa matukio muhimu ya binadamu vikiwamo vizazi na vifo.
Sheria ya Usajili wa Vizazi na Vifo Sura 108 Toleo la 2002 imempa mamlaka Msajili Mkuu kuthibitisha uhalali wa cheti cha kuzaliwa na cha kifo kulingana na kumbukumbu zilizopo katika Daftari la Msajili Mkuu.