Maeneo 4 yatajwa kuleta mageuzi sekta ya kilimo

MKURUGENZI wa Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti na Uendelezaji wa Kilimo Mashariki na Kusini mwa Afrika cha Mboga Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Dk Gabriel Rugalema, ameainisha maeneo makuu manne ambayo yakizingatiwa yatafanikisha mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo Tanzania.

Dk Rugalema ambaye taasisi yake makao yake makuu yapo jijini Arusha, aliwaambia waandishi wa habari waliotembelea kituo hicho kujifunza shughuli mbalimbali.

Alisema Tanzania ina nafasi kubwa ya kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo na kuchangia mafanikio kwenye sekta ya viwanda na kukuza uchumi.

“Uwekezaji wa ndani katika sekta ya mbegu ni muhimu katika mageuzi ya kilimo na kuinua uchumi. Kwa hiyo ni muhimu mkulima akawa na uhakika wa mbegu bora na za kutosha. Wakulima wengi wanashindwa kufikia malengo ya uzalishaji kwa sababu ya tatizo hili,” alisema.

Dk Rugalema aligusia pia suala la kubadilisha fikira za vijana kuhusu kilimo akitaka zifanyike juhudi za makusudi kuwafanya vijana kupenda kilimo kwa ajili ya maendeleo yao wenyewe.

“Na sisi tumeliona hilo na ndiyo maana tumeanzisha kituo cha ubunifu ambako vijana waliohitimu vyuo vya kilimo na vingine tunawapa mafunzo ya vitendo ili waweze kujiajiri au wanapoajiriwa kwenye kampuni zinazojihusisha na kilimo wawe na soko,” alisema.

Alisema vijana wengi wanamaliza vyuo lakini wanashindwa kushindana kwenye soko la ajira na pia wanashindwa kutoa mchango stahiki wanakoajiriwa. Alisema kuwa uzoefu umeonyesha kwamba vijana wanaopata mafunzo ya ubunifu katika taasisi yao wamebadilika kifikra na kiuchumi.

Eneo jingine ambalo Tanzania inapaswa kujielekeza ni kuzalisha mazao kulingana na masoko na kulingana na hali ya hewa ya sehemu tofauti nchini. “Katika kuleta mageuzi makubwa kwenye kilimo hili eneo lazima liwekewe mipango mizuri,” alisema.

Mratibu wa Mafunzo na Ugani wa taasisi hiyo, Hassan Mndiga, alisema kituo kimekwishatoa mafunzo kwa wakulima zaidi ya 4,000 kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya Tanzania.

Alisema kuna kipindi walikuwa wakitoa  mafunzo kwa wanafunzi kutoka zaidi ya nchi 20 kwa wakati mmoja. Alisema wengi wa wanafunzi waliopita ni wakurugenzi katika idara mbalimbali za serikali na sekta binafsi.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button