Maeneo yanayolalamikiwa kimaadili yatajwa

WAKATI utafi ti unaonesha hali ya uzingatiaji maadili katika utumishi wa umma imepanda kwa asilimia 75.9, maeneo matano yameonesha kulalamikiwa kukithiri kwa vitendo visivyo vya kiadilifu, ikiwemo Jeshi la Polisi, mahakama, manunuzi ya umma, mikataba na huduma za ardhi.

Hayo yalibainishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama wakati wa kutangazwa matokeo ya Utafiti wa Hali ya Uzingatiaji Maadili katika utumishi wa umma ya mwaka 2022.

Utafiti huo ulifanywa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 na uliendeshwa na Mtaalamu Mwelekezi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, Kampasi ya Dar es Salaam, Dk Francis Mwaijande.

Alisema matokeo ya utafiti huo yanaonesha kiwango cha uzingatiaji wa maadili kimeongezeka kwa wastani wa alama asilimia 9.8 kwa mwaka 2022 ikilinganishwa na asilimia 66.1 ya utafiti wa mwaka 2014.

“Lengo kuu la utafiti wa mwaka 2022 ilikuwa ni kubaini kama kumekuwa na ongezeko la uzingatiaji wa viwango vya maadili katika Utumishi wa Umma ambapo matokeo ni asilimia 76.9,” alisema.

Alisema utafiti unaonesha hali hiyo imechangiwa na juhudi za serikali za kuchukua hatua za kuweka misingi imara ya usimamizi wa maadili, kuweka mazingira wezeshi na kuimarisha uwajibikaji katika utumishi wa umma.

Jenista alisema katika utafiti huo, wadau 1,429 walihojiwa kwa kujibu dodoso, kati yao 793 (asilimia 55.5) walikuwa wanaume na 636 (asilimia 44.5) walikuwa wanawake.

“Aidha, ili kuhakikisha dhana ya usawa inazingatiwa wahojiwa 700 (asilimia 49) walikuwa ni wateja wa ndani ambao ni watumishi wa umma nchini na 729 ambao ni asilimia 51 walikuwa ni wateja wa nje ambao ni wananchi wasio watumishi wa umma,” alisema.

Alisema kwa mujibu wa matokeo ya taarifa hiyo, maeneo ambayo yamebainishwa kufanya vizuri ni eneo la dhamira ya uongozi katika kuimarisha utamaduni wa kiadilifu ndani ya utumishi wa umma na eneo la Tehama.

Aidha, Jenista alisema maeneo ambayo yamebainishwa na utafiti ambayo yanahitaji kuboresha au kutiliwa mkazo ni pamoja na ufuatiliaji wa kila mara wa uzingatiaji wa kanuni za maadili kwa watumishi wa umma.

Habari Zifananazo

Back to top button