Maeneo yenye changamoto usikivu wa redio kuboreshwa

Maeneo yenye changamoto usikivu wa redio kuboreshwa

WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye, ameahidi kukomesha utaratibu wa wananchi waishio maeneo ya pembezoni mwa nchi kusikiliza redio za nchi nchi jirani  na kwamba watakuwa wakisikiliza redio za ndani ya Tanzania.

Ameyasema hayo katika hafla ya uzinduzi wa kituo cha kurushia matangazo ya redio cha TBC Taifa na TBC FM yaliyofanyika Kata ya Inyonga, Wilaya ya Mlele mkoani Katavi.

Kauli hiyo imekuja baada ya maombi ya Mbunge wa Jimbo la Mpanda Vijijini Suleiman Kakoso na Mbunge wa Jimbo la Katavi, Isack Kamwelwe kuwa baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Nkasi, Tanganyika na Uvinza kwa asilimia kubwa hawasilikizi redio za ndani ya nchi.

Advertisement

Waziri Nape amesema serikali inatambua yapo maeneo nchini ambayo yamekuwa na changamoto ya usikivu wa redio hasa ya mipakani,  ambapo wamekuwa wasikiliza redio kutoka nchi jirani hizo.

 

“Nimekuja mipakani, nataka nihakikishie bunge kwa niaba ya wananchi na niwahakikishie wana Mlele na Katavi, tutakomesha utaratibu wa kusikiliza redio kutoka nchi jirani.

“Tunataka tuhakikishe majirani zetu kwa sababu nao wameanza kujifunza Kiswahili wanasikiliza TBC ndio maana tunataka tuimarishe, hilo ni agizo la Bunge, ni agizo la Rais Samia niko hapa kulitekeleza, kwa ziara hii nina hakika bajeti ijayo watatuongezea, ili twende sawa sawa,”amesema Waziri Nape.

Amesema tukio hilo ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya 2020-2025, ambayo inaeleza Serikali kuwekeza na kuimarisha miundombinu ya utangazaji ya TBC.

Ameipongeza TBC kushirikiana na UCSAF kufanikisha masafa mapya ya redio, huku akiwaomba wananchi wa Mlele kutunza miundombinu ya mnara wa matangazo kwa kuwa imejengwa kwa fedha za serikali zinazotokana na jasho la wananchi, hivyo ni mali yao.

Awali Mkurugenzi Mkuu wa TBC Dk Ayoub Rioba alisema kuwa mradi huo uliogharimu zaidi ya Sh bilioni 1, ulijumuisha ujenzi wa majengo kwa ajili ya mitambo na ununuzi wa mitambo yenyewe ya kurushia matangazo, ununuzi wa wa vifaa vya mifumo ya umeme (AVR na viyoyozi), mfumo wa kupokelea matangazo ya satellite na mfumo wa jenereta.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa mfuko wa mawasiliano kwa wote (UCSAF), Justina Mashiba amesema wameendelea kuhakikisha kuwa si mawasiliano ya simu pekee bali pia mawasiliano ya redio yanapatikana katika maeneo ya vijijini, mijini na pembezoni.

“Mpaka sasa tumesaini miradi ya kupeleka usikivu na kuboresha studio katika maeneo 15, ambapo tumeboresha studio ya TBC Dodoma na Studio ya Arusha kuwa za kisasa, tunaendelea na miradi ya kujenga vituo vya kurushia matangazo katika maeneo mengine yaliyobaki,” amesema Justina.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *