WADAU wa maendeleo wanaochangia utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) wamepongeza kazi nzuri inayofanywa kupitia miradi ya ajira za muda, kujenga uchumi wa kaya na uhawilishaji fedha wakisema wanaridhishwa na mafanikio wanayopata walengwa.
Wadau hao kutoka Benki ya Dunia, na ubalozi wa Uingereza na Ireland wameyasema hayo baada ya kutembelea baadhi ya wanufaika katika vijiji vya Ikangamwa na Ilamba wilayani Mufindi mkoani Iringa.
“Tuliamua kuinga mkono serikali ya Tanzania katika utekelezaji wa mpango huu wa Tasaf tukitambua kwamba unakwenda kuwasaidia walengwa kujikwamua kiuchumi na kuwapatia watoto wao mahitaji yao ya msingi,” anasema mwakilishi wa ubalozi wa Ireland, Mathew Cogan.
Cogan anasema Tasaf imeleta mabadiliko chanya katika maisha ya watu kwa kutoa huduma bora zinozohusiana na afya, elimu, miundombinu, na nyingine za kijamii kwa kaya masikinina nguvu kubwa inayooneshwa na wanawake walioko katika mpango huo katika kubadilisha maisha yao.
Naye Samuel Raff kutoka ubalozi wa UIngereza amewahimiza walengwa kutumia vizuri ruzuku yao ili wawe na kipato kitachowawezesha kumudu gharama za maisha pindi mradi utakapofikia tamati.
Naye Stanley Magesa kutoka Benki ya Dunia anasema wanaridhishwa na utekelezaji wa mpango na namna Tasaf ilivyofanikiwa kushirikisha na kutoa fursa kwa jamii kuchangia katika mchakato wa maamuzi na utekelezaji.
Magesa anasema miongoni mwa mambo waliyoyaona wakati wa ziara yao wilayani Mufindi ni pamoja na mpango kufahamika vizuri kwa walengwa na utekelezaji mzuri wa afua zote za mpango zilizopelekea walengwa kukidhi vigezo.
Mmoja wa wanufaika wa mpango huo, Shani William wa kijiji cha Ikangamwa anazungumzia jinsi miradi ya ajira za muda ilivyomuwezesha kupata Sh 350,000 alizozitumia kuanzisha mradi wa ufugaji wa kuku na mbuzi na kumuwezesha kufanya biashara ndogondogo na kilimo cha mahindi na mbogamboga ambavyo vyote kwa pamoja vimemuongezea mapato.
“Lakini pia Napata ruzuku ya Sh 24,000 kila baada ya miezi miwili; fedha hizo zinanisaidia kuwawezesha watoto wangu watatu kupata baadhi ya mahitaji yao muhimu ikiwa ni pamoja na matibabu yao,” anasema William.
Naye Maneno Kassim alitoa taarifa ya mradi wa upandaji miti uliotekelezwa na walengwa wa Tasaf katika kijiji cha Iramba.
Kassim ambaye ni msimamizi wa mradi huo ulioamzishwa mwaka 2023 aliwaambia wadau hao wa maendeleo kwamba miti hiyo zaidi ya 9600 imependwa katika shamba lenye ukubwa wa ekari 15 na kwamba itakapofikia muda wa kuvunwa na kuuzwa, mapato yake yatatumika kuchochea maendeleo ya walengwa 52.
“Miaka kadhaa imepita tangu familia nyingi zilizokuwa zikiishi katika lindi la umasikini na kukataa tamaa ya maisha ziingizwe katika mpango wa kunusuru kaya mkoani Iringa” anasema Mratibu wa Tasaf Mkoa wa Iringa, Saida Mgeni.
Mgeni anasema; umaskini ni pengo kati ya rasilimali na mahitaji; “na hautafsiriwi kwa ukosefu wa rasilimali na mapato pekee- lakini pia na gharama ya kupata mahitaji mbalimbali ya msingi.”
Anasema Tanzania iliamua kupitisha na kutumia Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA) wenye misingi ya Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) inayozingatia matokeo ili kuendeleza mafanikio yaliyofikiwa na kukabiliana na changamoto za kukuza uchumi na kupambana na umaskini.
“Malengo ya Maendeleo ya Milenia au MDGs yaliundwa mwaka 2000 yakilenga kupunguza umaskini kwa nusu ifikapo mwaka 2015. Mwaka 2015, mpango mwingine wa miaka 15 uliundwa kwa ajili ya kutekeleza malengo hayo ya maendeleo endelevu au SDGs ifikapo mwaka 2030,” anasema.
Mkurugenzi wa Uratibu wa Tasaf, Haika Shayo anasema mwaka 2000 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilianza kutekeleza mpango huo ikiwa ni moja ya mbinu za kutokomeza umasikini ambazo pia zilisaidia ajenda ya ugatuaji wa madaraka.
Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi Michael Haule aliishukuru serikali na wadau wake wa maendeleo kwa kutekeleza mpango huo akisema umebadili maisha ya wananchi wengi waliokuwa wanakabiliwa na umasikini wa kupindukia.