MKUU wa Wilaya ya Tanganyika, Onesmo Buswelu amewataka wakulima wa korosho wilayani humo, kutumia maarifa na ujuzi katika suala la utunzaji, ili waongeze tija.
Buswelu ametoa rai hiyo kwenye utolewaji mafunzo kwa wakulima wa korosho, namna ya uzalishaji, utunzaji na unyunyiziaji viuatilifu yaliyofanyika Kijiji cha Kabungu.
Amesema wakulima wanatakiwa kutumia weledi katika kilimo hicho na kwamba wanahitaji kufanya ufuatiliaji wa karibu na serikali na taasisi zinazohusika, ili wapate korosho bora.
“Maofisa Ugani mliopo hapa, hakikisheni elimu hii mnaifikisha kwa wakulima na tunahitaji kuona muunganiko kutoka bodi ya korosho, ikisimamia kwa ukaribu kilimo hiki,” amesema Buswelu.
Wadau wa mafunzo hayo Bodi ya Korosho Tanzania, Kampuni ya Bens Agro Star na watafiti wa kilimo kituo cha Naliendele, walisema changamoto kubwa inayowakabili wakulima ni elimu duni ya kilimo hicho.
“Walikuwa hafahamu kudhibiti magonjwa na wadudu waharibufu na katika matumizi ya viuatilifu, walishindwa kufahamu ni kiuatifu gani kitumike,” amesema Dk Julius Nambua kutoka Bens Agro Star.
“Wakulima pia hawafahamu utambuzi wa viuatilifu vya kudhibiti na kuua wadudu, lakini wataalamu wa kilimo hawana uelewa wa kutosha kuhusu korosho,”amesema Bobmary Asenga mtafiti Naliendele.
Ofisa Kilimo kutoka bodi ya korosho Tanzania, Samweli Kambona, amesema hali ya uzalishaji wa korosho Katavi inaridhisha.
“Ukanda huu wakulima wanahitaji elimu ya kutosha kwenye matumizi sahihi ya viuatilifu na unyunyiziaji, mafunzo haya yatawasaidia, kiwanda cha kubangua korosho kimeanza kujengwa,” amesema Kambona.
Wakulima wa korosho Wilaya ya Tanganyika, Malale Kausimbe na Christina Lugenzi, walisema walikuwa hawana elimu juu ya kilimo hicho, hivyo kusababisha mazao yao kushambuliwa na magonjwa.