DODOMA: MKURUGENZI wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi amesema hadi sasa nyumba zaidi ya 100 zimepotea kutokana na mafuriko yaliyotokea Hanang na kusababisha vifo vya watu 87 na majeruhi 137.
Matinyi ameyasema hayo leo jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) uliofanyika Dodoma na kukutanisha viongozi wa vilabu 28 vya waandishi wa Habari nchini.
Amesema miamba laini ya milima ya Hanang ililowa nakutengeneza tope wakati wa mvua na hivyo kushuka na kuzibua banio la maji na kupelekea maafa.
Amesema timu ya wataalamu walichukua picha za sateliti kabla ya tukio kutokea na baada ya tukio hilo kutokea na baadaye wataalam wa Sensa ya Watu na Makazi wametoa matokeo ya sensa waliyoyafanya katika eneo hilo lililokumbwa na mafuriko na kubaini nyumba zaidi ya 100 hazipo yakiwemo maduka na soko.
Amesisitiza kuwa wataalamu wa miamba wamefanya uchunguzi na kuweka alama katika eneo hilo na kusema kitaalamu kuwa eneo hilo si salama kwa makazi na maisha ya mwanadamu kwahiyo watu watahama eneo hilo