RUFIJI: Chanzo cha mafuriko Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani kimetajwa kuwa ni uvamizi wa wananchi katika mkondo wa mto na kufanya shughuli za kibinadamu.
Hayo yamesemwa na Mhandisi wa Tanesco, Dismass Mbote katika ziara ya maalum ya Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana alipotembelea waathirika wa mafuriko Rufiji.
Amesema kiwango cha maji katika Mto Rufiji kimewahi kurekodiwa ni mita za ujazo 13,000 kwa sekunde. Kiwango hicho kilirekodiwa mwezi Mei mwaka 1974, lakini kiwango cha maji yanayotiririka katika mto Rufiji kwa mwezi Machi na Aprili ni mita za ujazo 8,444 kwa sekunde.
“Maana yake ni kwamba kiwango cha maji Mto Rufiji kwa mwaka huu hakijafikia makadirio ya juu kama ilivyokua mwaka 1974. Sasa kwa nini mafuriko yametokea?” Amehoji na kuongeza:
“ Kwa nini kiwango cha mita za ujazo 13,000 mwaka 1974 hakikusababisha madhara makubwa kama kiwango cha mita za ujazo 8,444 mwaka huu? Jibu ni kwamba wananchi wamevamia eneo la mkondo wa mto na kufanya shughuli za kibinadamu ikiwemo kulima na kujenga.”
Amesema, serikali ilipoanza kujaza maji kwenye Bwawa la Julius Nyerere mwaka 2022 maji yote ya Mto Rufiji yalizuiwa, kwa hiyo hakukua na maji yaliyotiririka kuelekea bahariani, matokeo yake wananchi walisogea kwenye mkondo wa mto na kuanza kufanya shughuli za kibinadamu ikiwemo kilimo na makazi, jambo ambalo ambalo limeongeza athari.
Amesema mvua za El Nino zinazoendelea kunyesha ambazo zimesababisha mafuriko katika baadhi ya maeneo kama Rufiji, Kilombero, Mvomero, Kilosa, Mlimba, Liwale na Mbarali ukiacha Rufiji maeneo hayo yameathirika na mafuriko wakati hayajapitiwa na Bwawa la Nyerere.
Kwa mujibu wa mtaalamu huyo amesema mwaka 1997, 2000, 2003, 2011, 2016 na 2020 wilaya hiyo ilikumbwa na mafuriko makubwa yaliyosababisha uharibifu wa mali na baadhi ya watu kupoteza maisha wakati huo Bwawa la Nyerere halikuwepo, kwa hiyo kueleza kwamba bwawa hilo limesababisha mafuriko si kweli.