MOROGORO; KAYA 179 zinazoishi Kijiji cha Taweta , Kata ya Masagati , wilaya ya Kilombero , mkoani Morogoro zimekosa mahala pa kuishi kutokana na nyumba zao kuingiliwa na maji na nyingine kubomoka kufuatia mvua za mafuriko zilizonesha kuanzia juzi.
Diwani wa Kata ya Masagati, Blasius Makao amesema hayo leo Aprili 3,2024 kwa njia ya simu kuwa mvua hizo zilianza Aprili Mosi mwaka huu na zimenyesha kwa siku mbili mfululizo.
Amesema nyumba 15 zimepata madhara makubwa na kati ya hizo saba zimebomoka na ziliosalia hazina uwezo wa kuhimili kubakia salama, kwani zimeathiriwa vibaya .
Amesema kulingana na kaya hizo, watu wake 895 hawana uwezo kwenda kuishi katika nyumba zao kutokana na kuingiliwa na kiwango kikubwa cha maji.
“Kwa sasa Kata ya Masagati imezingirwa na maji ya mvua za mafuriko kutoka Aprili 1 mwaka huu hadi ninavyoongea leo ( Aprili 3, 2024…watu wanaishi uhamishoni kwenye ofisi ya serikali ya kijiji, ofisi ya kata na kwenye shule, “ amesema Makao.
Amewaomba wadau mbalimbali kujitokeza kusaidia waathirika hao kwa chakula , mavazi na mahitaji mengine ya kibinadamu katika kipindi hiki kigumu kwao.
Viongozi wa serikali ya mkoa pamoja na Wilaya ya Kilombero wameelekea katika Kata ya Masagati kwa kutumia usafiri wa anga, ili kujionea hali halisi na namna ya kuchukua hatua mbalimbali za kuwapatia msaada waathirika wa mafuriko hayo.