TAKRIBANI watu 95 wamekufa Magharibi mwa Taifa la Rwanda kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa.
François Habitekeko, Gavana wa Mkoa wa Magharibi wa Rwanda amethibitisha idadi hiyo ya vifo.
“Mvua kubwa ilinyesha usiku kucha na kusababisha adha kubwa katika Wilaya za Ngororero, Rubavu, Nyabihu, Rutsiro na Karongi,” alisema Habitekeko.
Wilaya zilizoathirika zaidi katika jimbo hilo ni Rutsiro, ambako watu 26 walikufa, Nyabihu na 19, Rubavu na Ngororero vifo 18 kila moja, aliongeza.
Habitekego amesema mvua ilianza saa kumi na mbili jioni (16:00 GMT) siku ya Jumanne na Mto Sebeya ulipasua kingo zake.
“Udongo ulikuwa tayari umelowa kutokana na mvua ya siku zilizopita, ambayo ilisababisha maporomoko ya ardhi ambayo yalifunga barabara,” aliongeza gavana huyo.
Kipande cha video kilichotumwa kwenye akaunti ya Twitter ya Shirika la Utangazaji la Serikali ya Rwanda kilionyesha maji ya matope yanayotiririka kando ya barabara na nyumba zilizoharibiwa.