Magandi: Virutubisho kunusuru vichwa vikubwa, mgongo wazi

DAR ES SALAAM: WANAWAKE wajawazito wametakiwa kutumia virutubisho ili kuwanusuru watoto kuzaliwa na tatizo la vichwa vikubwa na mgongo wazi.

Hayo yamesemwa leo Machi 7, 2024 na Naibu Mkurugenzi wa Hospitali ya Muhimbili Mloganzila, Dk Julieth Magandi wakati akipokea vifaa mbali mbali pamoja na kiasi cha pesa za matibabu kutoka kwa  watumishi wanawake wa Bohari ya Dawa (MSD) ikiwa ni kuelekea maadhimisho ya siku ya wanawake duniani kesho Machi 8, 2024.

Dk Magandi amesema, ugonjwa wa mgongo wazi au vichwa vikubwa unaweza kumkumba mtoto yeyote ambaye mama yake hakupata virutubisho alivyotakiwa kuvipata  kabla ya kushika mimba.

Advertisement

Anasema kwa kawaida virutubisho hivyo vinapatikana katika vyakula vyote vyenye protini na vina uwezo wa kumzuia mama kwa asilimia kubwa asipate changamoto ya kuzaa mtoto mwenye ulemavu wa mgongo wazi na kichwa kikubwa.

“Ugonjwa wa mgongo wazi au (spinal bifida) na vichwa vikubwa ni ulemavu anaozaliwa nao mtoto na akishaupata matibabu yake ni upasuaji wa haraka ili kuzuia tatizo lisiendelee na katika hatua hii mama anatakiwa kumuwahi pindi anapozaliwa tu afanyiwe matibabu,”amesema.

Dk Magandi amesema gharama za matibabu hususani kwa watoto wenye changamoto za matibabu ya mgongo wazi na vichwa vikubwa ni kubwa na watu wengi hawawezi kuzimudu kama hawana bima ya afya na hivyo kuwaomba wadau kuendelea kujitokeza kuwasaidia ili kurudisha tabasamu la watoto hao.

“Kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji Prof. Mohamed Janabi napenda niwashukuru na kuwapongeza kwa kuona umuhimu katika kuelekea Siku ya Wanawake Duniani, mkaona mje Mloganzila kwa kutumia sehemu ya mapato yenu binasi kutoa sadaka kwa kuwashika mkono wanawake wenzenu ambao watoto wao wana mahitaji na kwa uwezo wao hawawezi kumudu gharama za matibabu,” amesema Magandi

“Wasichana wengi hivi sasa wamekuwa wakijifungua watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi kwa sababu wamekuwa wakishika ujauzito huku wakiwa hawajui kama wana upungufu wa madini ya folic acid,” anasema.

Anasema ili mama aweze kuepuka kuzaa mtoto mwenye kichwa kikubwa na mgongo wazi anatakiwa kabla ya kushika mimba ale vyakula vyenye protini kama mayai, mboga mboga, maziwa, mahindi, maharage, parachichi, embe na kadhalika

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wanawake MSD, Rehema Mosha amesema wanawake wa MSD wameamua kuadhimisha siku ya wanawake mwaka huu kwa kulipia sehemu ya matibabu ya watoto wenye changamoto ya mgongo wazi na vichwa vikubwa ambao matibabu yake  yamekuwa na gharama kubwa.

Amesema, pamoja na kulipia sehemu ya gharama za matibabu pia wametoa misaada midogo midogo ikiwemo dawa za meno, pampasi, sabuni na wipers ambazo zitawasaidia katika usafi wa watoto hao pindi wawapo wodini.