‘Magari ya Zimamoto yapishwe barabarani’

JESHI la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mwanza limewataka watumiaji wa barabara kupisha magari yao yanapokuwa yanakwenda kukabili majanga ya dharura yanapotokea ili kuepusha ajali zisizokuwa za lazima.

Hayo yamebainishwa jana jijini hapa na Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mwanza, Kamila Labani katika mahojiano maalumu na HabariLEO juu ya utendaji kazi wa jeshi hilo katika kukabili majanga ya dharura.

Kamanda Labani alisema kuwa changamoto kubwa ni uelewa mdogo kwa watu wanaotumia barabara kushindwa kupisha magari yao kwa wakati wanapokwenda kwenye matukio kwa kuwa magari yao hukimbia kwa haraka kuwahi eneo la tukio.

Kamanda Labani alisema Sheria ya Usalama barabarani kifungu Namba 54 ya mwaka 1973 ambayo ilifanyiwa marekebisho mwaka 2002 na mwaka 2022, inabainisha hitaji la kupishwa kwa magari hayo wakati wa dharura.

“Japo magari yetu kwa nyakati za matukio ya dharura hupiga ving’ora lakini bado baadhi ya madereva na watumiaji wa barabara hushindwa kutoa ushirikiano kwa kutupisha,” alisema.

Alisema Sheria ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ya mwaka 2007 namba 14 kifungu cha 12 namba 1, 2 na 3, inataka magari ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji  kupishwa na magari yote ili waweze kuokoa maisha na mali hasa katika matukio ya dharura.

Alisema kuwa ruhusa iliyotolewa na kifungu hicho cha sheria kwa magari ya dharura itatumika pale dereva wa gari hilo awapo kwenye mwendo atakuwa anapiga king’ora au filimbi kadiri inavyowezekana au pale ambapo gari litakuwa na kimulimuli atawasha kwa wakati wote hivyo kuonekana umbali wa meta 150 kutoka mbele ya gari.

Habari Zifananazo

Back to top button