Magereza, shule zatakiwa kutopikia kuni

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Dk Suleman Jafo amezitaka shule, magereza na kambi za jeshi kuanza kuachana na matumizi ya kuni na mkaa kuokoa rasilimali za misitu.

Alisema kutokana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na maendeleo ya sayansi na teknolojia, imefika wakati sasa kwa taasisi hizo kuanza kutumia nishati mbadala yenye athari ndogo katika mazingira.

Jafo alitoa maelekezo hayo juzi alipozungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea maonesho ya tano ya teknolojia ya madini yanayoendelea viwanja vya Bombambili mjini Geita.

“Jambo la kwanza tuanze kuhakikisha kwamba tunawekeza katika matumizi ya biogesi. Bahati nzuri kwa taasisi hizi suala la matumizi ya biogesi ambayo ni kinyesi cha binadamu kinapatikana kwa wingi zaidi,” alisema.

Aliongeza: “Sasa watumie mfumo rafiki zaidi, wanaweza kutumia biogesi, ama kama wanatumia mkaa basi watumie mkaa mbadala. Naamini hata taasisi hizi zikiamua zenyewe zianzishe mitambo ya kutengeneza mkaa mbadala zinaweza.”

Alisema serikali inafurahi kuona Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) likijielekeza katika utengenezaji wa mkaa mbadala ambao unatokana na makaa ya mawe. “Tumeona sasa changamoto hii ya matumizi ya kuni na mkaa inaondoka.”

Meneja Uhusiano wa Stamico, Geofrey Meena alisema kwa sasa wamejikita kutoa elimu na kutangaza mkaa mbadala unaofahamika kama ‘rafiki brick’ ili kutengeneza soko la uhakika nchi nzima.

Meena alisema mwamko wa matumizi ya mkaa mbadala yatawezesha kuokoa asilimia kubwa ya miti inayopotea kila mwaka kutokana na matumizi ya mkaa na kuni na kuirejesha Tanzania ya kijani.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button