Mageuzi yaja usimamizi kwa mashirika ya umma

MSAJILI wa Hazina, Nehemia Mchechu ametangaza mageuzi katika ofisi yake, taasisi, mashirika ya umma na wakala wa serikali ili kuongeza ufanisi utakaoongeza mapato ya serikali.

Pamoja na hayo, Mchechu ameagiza kuwa ifikapo mwakani itakuwa ni lazima kwa taasisi hizo kutoa kwa umma taarifa za ripoti za utendaji za kila mwaka.

Mchechu alisema hayo Dar es Salaam jana alipozungumza na watendaji wakuu na wenyeviti wa bodi wa taasisi, mashirika ya umma na wakala za serikali.

Alitaja mageuzi ndani ya Ofisi ya Hazina yatakayofanyika kuwa ni kutengeneza mpango mkakati wa muda mrefu (zaidi ya miaka 10) unaoakisi malengo makuu ya taasisi na kufanya marekebisho ya Sheria ya Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sura 370 kwa kuwa ina migongano na baadhi ya sheria za nchi na hivyo kuathiri utekelezaji wa majukumu yake kikamilifu na kwa tija.

“Pia ofisi yetu imejipanga kuimarisha ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi kutoka Sh bilioni 637.64 mwaka 2020/21 kwenda shilingi trilioni 1.2 na zaidi ifikapo mwaka 2025/26,” alisema Mchechu.

Alitaja mageuzi mengine kuwa ni kuanzishwa kwa Mfuko wa Uwekezaji ambao utakuwa na fedha kwa ajili ya uwekezaji na kuwezesha mitaji kwa taasisi.

Mchechu alitaja mageuzi mengine ni kutambua mashirika yanayopaswa kujiendesha kibiashara na kwa faida na kuyawezesha kimtaji ili yajiendeshe yenyewe bila kutegemea ufadhili wa serikali.

Mageuzi mengine ni kuboresha mashirika na taasisi za umma kwa kufanya uchambuzi wa kina wa mashirika hayo ili ufanisi uakisi kama ni ya kibiashara au huduma, kuimarisha uwezo wa bodi za wakurugenzi na kuratibu mamlaka kufanya mabadiliko ya sheria na miongozo ili ziweze kutoa maamuzi na kuyasimamia.

Mchechu alisema Ofisi ya Msajili wa Hazina inatarajia kuwa mashirika hayo ya umma yatafanya mageuzi ili kuwa na tija katika uchumi na kuonesha umuhimu wa kuanzishwa kwake.

Aliagiza taasisi hizo zipitie na kuhuisha mpango mkakati wa taasisi husika na maandiko ya kibiashara na kupendekeza mabadiliko katika sheria ili kuondoa mapungufu yaliyopo.

“Kila taasisi inapaswa ijitathmini na ichangie gawio serikalini. Kwa sasa hali sio nzuri ya uchangiaji nyingi hazichangii. Takwimu zinaonesha mwaka 2019/20 taasisi 236 zilichangia gawio, mwaka 2020/21 taasisi 200 zilichangia wakati mwaka 2021/22 ni taasisi 136 tu ndio zilichangia. Hizi taasisi 60 na zaidi zimekwenda wapi?” Alihoji.

Alitaka uchangiaji wa gawio usilazimishwe bali taasisi hizo ziweke mipango na mikakati thabiti ya kiutendaji ili zizalishe kwa faida ndipo zichangie.

“Haitakuwa na maana taasisi leo itoe gawio la shilingi bilioni mbili serikalini halafu kesho ianze kuomba kusaidiwa hazina,” alisema Mchechu.

Pia, alizitaka taasisi hizo ziimarishe uhusiano wa kiutendaji ndani ya taasisi moja na nyingine, zifanye kazi kwa weledi, ubunifu, zizingatie misingi ya utawala bora na ziwe na utayari kunapotokea majanga yatakayolikumba Taifa.

Kuhusu ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), alizionya taasisi ambazo zimekuwa zikirudiwa kutajwa kwenye ripoti hizo na kuagiza taasisi na mashirika yote kuhakikisha wanafunga hesabu ipasavyo.

“Lakini ni wajibu wetu na sisi kuzungumzia yale mazuri tunayoyafanya. Ripoti hii ya CAG ikitoka bahati mbaya wengi wenu mnakuwa maarufu kwa mabaya. Tumieni taarifa zenu za utendaji za mwaka au ripoti za fedha kuelezea mafanikio yenu kama benki zinavyofanya,” alisema Mchechu.

Habari Zifananazo

Back to top button