Magonjwa yasiyoambukiza mzigo, vyanzo vyatajwa

Magonjwa yasiyoambukiza mzigo, vyanzo vyatajwa

WIZARA ya Afya imesema magonjwa yasiyoambukiza ni mzigo kwa taifa na kwamba uzito kupita kiasi, unene uliopitiliza vinasababisha asilimia 73 ya magonjwa hayo.

Imetaja vichocheo vingine ni changamoto za lishe zinazosababisha magonjwa hayo kwa asilimia 32 na matumzi ya tumbaku kwa asilimia 14.8.

Mkurugenzi wa Magonjwa yasiyoambukiza kutoka Wizara ya Afya, Dk James Kiologwe alisema hayo jana alipozungumza kwenye semina kwa njia ya mtandao kuwajengea uwezo waandishi wa habari.

Advertisement

“Mzigo wa magonjwa umeongezeka nchini na vihatarishi vimeongezeka kwa kasi hivyo tunatakiwa kungalia nini cha kufanya kudhibiti hili,” alisema Dk Kiologwe.

Aliongeza: “Sasa watu wanaofanya ngono isiyo salama ni wachache kuliko wenye uzito kupindukia, mzigo unaongezeka, theluthi mbili hawajifahamu, wengine wanafika hospitali wakiwa na madhara zaidi.”

Alisema tafiti zinaonesha kuwa kwa miaka 10 visababishi vimeongezeka kwa magonjwa yasiyo yakuambukiza kuliko ya magonjwa ya kuambukiza.

Dk Kiologwe alisema vihatarishi vinavyosababishwa na lishe isiyo sahihi ni asilimia 18 huku vihatarishi vya matumizi ya pombe ikiwa ni asilimia 15.9.

Alisema kuna haja ya kutoa elimu zaidi kwa jamii ili ichukue kukabili magonjwa hayo.

“Tumeona kuna haja sana ya kupata elimu kwa magonjwa yasiyoambukiza, tumeamua kutumia mhimili wa habari ili kutoa elimu sahihi na katika mapambano haya tunakinzana na changamoto za kibiashara na viwanda ambazo nao ni muhimu kupata elimu sahihi,” alisema.

Dk Kiologwe alisema wanatengeneza timu kwa kila mkoa ili kutoa elimu ya magonjwa yasiyoambukiza na wanatarajia kuandaa tuzo kwa wanaoandika habari zinazohusu magonjwa hayo.

Alisema tabia bwete, ulaji usiofaa na kutokufanya mazoezi ni vyanzo vikubwa vya magonjwa hayo.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2016, zinaonesha kuwa vifo milioni 42 sawa na asilimia 71 vilivyotokea duniani vilitokana na magonjwa hayo na asilimia 25 ya vifo hivyo vilihusu umri wa miaka 30 hadi 70.