WABUNGE wamekubali kuanzishwa kwa mahabusu zinazojitegemea na maalumu kwa ajili ya watuhumiwa wa dawa za kulevya.
Hayo yamo katika Muswada wa marekebisho ya Sheria ya kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Sura ya 95 iliyopitishwa bungeni jana.
Vilevile wabunge kwa kupitisha Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali Na.2 wa mwaka 2022, wamekubali uwapo wa adhabu kali kwa watu watakaokutwa na hatia ya kusafirisha binadamu.
Bunge juzi lilijadili na kupitisha Muswada wa Sheria ya Kuzuia Usafirishaji Haramu wa Binadamu, Sura ya 432 na Sheria hiyo inaongeza adhabu katika vifungu vya 4, 5, 6, 7, 8A na 13 vya sheria hiyo.
Mbunge wa Viti Maalumu, Salome Makamba (Chadema), alisema tatizo la dawa za kulevya ni kubwa na kuwa matajiri wakubwa ndio wanaohusika kwa kushirikiana na mfumo.
Alisema kukamatwa watuhumiwa ni mchakato na wengine wanatoroka na ndio maana kuna haja ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kuwa na mahabusu zake ili watuhumiwa wawe katika maandalizi maalumu.
Kwa upande wa usafirishaji wa binadamu alipendekeza adhabu ya kifungo na faini iongezeke na kiwe kifungo cha maisha jela, akisisitiza kuwa wanaofanya biashara hiyo wanalipwa fedha nyingi za kigeni, kwa hiyo faini ya Sh milioni 50 kwao si kitu na wanaweza kulipa.
Mbunge wa Madaba, Dk Josephat Mhagama akichangia alisema madhara ya dawa za kulevya ni makubwa kwa vijana wengi ambao ni nguvu kazi ya taifa hivyo inatakiwa nguvu kubwa kudhibiti biashara hiyo.
Dk Mhagama alisema hoja ya mamlaka kuwa na mahabusu zake ni ya msingi kwa sababu katika mahabusu za polisi kuna mchanganyiko mkubwa na hivyo anakubaliana na pendekezo la serikali mamlaka hiyo kuwa na mahabusu zake.
Mbunge wa Manyoni Magharibi, Yahya Maswe alisema muswada huo umezingatia maslahi mapana ya taifa na kuwa biashara ya kusafirisha binadamu imeshamiri, hivyo udhibiti zaidi unahitajika ikiwa ni pamoja na adhabu kali.
“Sheria hii inakuja kuweka adhabu kali sasa kwa wale wanaorudia kosa hili la kusafirisha binadamu na lengo ni kuhakikisha hayajirudii tena… biashara hii inakwenda kudhibiti na kumaliza tatizo na kufifisha wafanyabiashara hii haramu kwa maslahi mapana ya nchi,” alisema.
Awali Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Najma Giga akiwasilisha maoni ya kamati alisema wameishauri serikali katika mahabusu ambazo zitaanzishwa katika mapendekezo ya muswada, ihakikishe inaweka masharti ambayo yatahakikisha watuhumiwa wanapata haki zote za msingi na kupata ulinzi unaostahili kwa mujibu wa sheria za nchi na hakijinai.
Najma alisema pia kamati imependekeza serikali ishirikishe Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika jitihada za kupambana na biashara ya dawa za kulevya.