Mahakama kutoa hukumu ushindi wa Ruto

Mahakama kutoa hukumu ushindi wa Ruto

MAHAKAMA Kuu ya Kenya leo inatarajiwa kutoa hukumu ya kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa Rais wa nchi hiyo uliofanyika Agosti 9 mwaka huu.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Wafula Chebukati alimtangaza William Ruto kuwa mshindi kwa kupata kura 7,176,142 sawa na asilimia 50.48.

Chebukati alisema kwenye ukumbi wa Bomas kuwa mgombea kupitia Muungano wa Azimio la Umoja, Raila Odinga alishika nafasi ya pili kwa kupata kura 6,942,930, sawa na asilimia 48.85.

Advertisement

Alisema Waihika David Maore alipata kura 31,907 sawa na asilimia 0.23 na Profesa Wajackoyah George alipata kura 61,969 sawa na asilimia 0.44.

Odinga aliwasilisha ombi katika Mahakama Kuu ya Kenya akipinga kutangazwa Dk Ruto kuwa Rais Mteule wa taifa hilo.

Katika wasilisho la hoja za kisheria lenye kurasa 70, mwanasiasa huyo anadai kuwa kulikuwa na njama za kubadili matokeo ya uchaguzi huo.

Jopo la mawakili 46 wa Odinga wakiongozwa na James Orengo na wakili wa Muungano wa Azimio, Daniel Maanzo, waliwasilisha malalamiko hayo kwa njia ya mtandao.

Katika maombi yao, mawakili hao waliiomba mahakama kumwamuru Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, George Kinoti atoe taarifa, picha, ripoti, vifaa kompyuta mpakato na simu na vifaa vingine vinavyohusishwa na uchaguzi.

Pia waliomba mahakama imuamuru Kinoti awasilishe kompyuta mpakato iliyochukuliwa kutoka kwa Wakala wa Chama cha UDA, Koech Geoffrey na pia kuitishwa kwa uchaguzi mpya ambao hautakuwa chini ya Mwenyekiti wa sasa wa IEBC, Wafula Chebukati pamoja na kupitiwa upya kwa fomu za matokeo za 34A, 34B na 34C.

Jeshi la Polisi nchini humo limehimiza wananchi wawe watulivu na limeshauri waache kuhama kutoka maeneo walipo kwa hofu ya kutokea vurugu.

Taarifa ya Kaimu Mkuu wa Polisi wa nchi hiyo, Noor Gabow ilieleza kuwa jeshi hilo limeimarisha ulinzi kwenye maeneo yote na amewahakikishia Wakenya na watu wengine kuwa watakuwa salama.

Gabow alishauri wananchi wasiende kukusanyika Mahakama Kuu na badala yake wafuatilie hukumu hiyo wakiwa nyumbani na akasema barabara zote zinazokwenda kwenye jengo la mahakama hiyo zitafungwa.