Mahakama kutoa uamuzi maombi ya nduguze Mtemvu

KITUO Jumuishi cha Mahakama cha Utoaji Haki kuhusu masuala ya kifamilia cha Temeke mkoani Dar es Salaam, kesho kinatarajia kutoa uamuzi wa maombi yaliyowasilishwa na ndugu wawili wa Mbunge wa zamani wa Temeke, Abbas Mtemvu.

Ndugu hao, Ibrahim na Jasmine Mtemvu wanaiomba mahakama hiyo itoe amri ya kuondoa uzio wa mabati na walinzi waliowekwa na Abbas kwenye nyumba iliyopo Kitalu Namba 1036/2 Haile Selassie, Masaki Kinondoni.

Oktoba 7, mwaka huu, Ibrahim na Jasmine walifungua shauri dogo wakiiomba mahakama hiyo kuwa Abbas aende kujieleza mahakamani hapo kwa nini asifungwe kwa kuendelea kuidharau amri ya mahakama kwa kuendelea kuwafukuza wanandugu hao kwenye nyumba hiyo ya urithi iliyoachwa na mama yao mzazi.

Mbali na hilo, ndugu hao ambao ni wadogo wa mbunge huyo wa zamani wa Temeke, wanaiomba mahakama iamuru utekelezaji wa amri iliyotolewa Oktoba 4, mwaka huu katika maombi ya mirathi namba 122/2022 kwa kumtaka Abbas kuwarudisha na kutowawekea vikwazo waleta maombi ya wapangaji wao ili waendelee na matumizi ya nyumba hiyo ya Masaki.

Wakili wa Kujitegemea anayewawakilisha Ibrahim na Jasmine, Ramadhan Karume aliieleza mahakama hiyo mbele ya Hakimu Simon Swai kuwa amri ya Oktoba 4, mwaka huu ya kuzuia waleta maombi wasitolewe na shughuli zinazofanyika kwenye nyumba hiyo ziendelee kama kawaida, lakini Abbas amekiuka amri hiyo.

Karume alidai wakati wanasubiria utekelezaji wa maombi hayo, wameiomba mahakama kwa njia ya mdomo itoe maelekezo ya kuondoa uzio wa mabati yaliyowekwa kwenye nyumba hiyo pamoja na kuwaondoa walinzi waliowekwa na Abbas.

“Hivyo mahakama haibanwi kutoa maamuzi kutokana na mazingira tajwa, hivyo tunaiomba mahakama hii iridhie maombi yetu tuliyotoa,” alidai Karume.

Wakili wa Kujitegemea anayemwakilisha Abbas, Nestory Wandiba aliiomba mahakama isitoe amri hadi atakapoleta kiapo kinzani ili shauri liendelee ili lisikilizwe pande zote.

Wandiba alidai Oktoba 4, mwaka huu mahakama hiyo ilitoa amri kwa upande mmoja huku mjibu maombi hakuwepo mahakamani hapo hivyo ameomba apewe haki ili apeleke utetezi wake kwa amri iliyotolewa.

“Tupewe muda ili tulete kiapo kinzani kwa kuwa ni haki yangu ili nieleze hao wapangaji ni kina nani na wanasema nyumba imewekwa mabati, hivyo vyote vinavyoongelewa hapa mahakamani naviona ni vipya,” alidai Wandiba.

Inadaiwa kuwa Abbas ameuza nyumba hiyo ya Barabara ya Haile Selassie Masaki, kwa Mustafa Mohamed ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Delligent Group kwa gharama ya Sh milioni 900 na amezitumia peke yake.

Mbali na Ibrahim na Jasmine, warufani wengine ni watoto watano wa kaka zao wawili, George Mtemvu na Modibo Mtemvu na wa dada yao Amina Mtemvu ambao ni marehemu.

Ibrahim na Jasmine wamemkatia rufaa ndugu yao Abbas wakipinga uteuzi wake kuwa msimamizi wa mirathi ya marehemu mama yao Sitti Kilungo kuwa ulikuwa si halali.

Abbas aliteuliwa kuwa msimamizi wa mirathi hiyo na Mahakama ya Mwanzo Temeke katika shauri la mirathi namba 474 la mwaka 2017 alilolifungua hapo.

 

Habari Zifananazo

Back to top button