Mahakama Kuu yafuta hukumu kesi ya uchawi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Iringa imefuta hukumu ya kifungo cha miaka mitano jela iliyotolewa na Mahakama ya Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe, baada ya mahakama hiyo kumtia hatiani John Severini Chale (60) kwa makosa ya kujihusisha na vitendo vya ushirikina.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Dk John Utamwa alitoa uamuzi huo baada ya kuona taarifa ya hukumu hiyo iliyotolewa Agosti 29 mwaka huu.

Katika nakala ya hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu baada ya kupitia jalada ya kesi ya John Chale, Jaji Dk Utamwa ameelezea mambo kadhaa yaliyozingatiwa kufuta hukumu ya kifungo cha miaka mitano jela na kuamuru mtuhumiwa huyo aachiwe huru na jadala la kesi hiyo lifutwe.

Jaji Dk Utamwa alipitia mambo kadhaa ya utaratibu wa kufungua jalada la kesi na kuangalia kama sheria ilizingatiwa na iwapo ushahidi wa kutosha ulipatikana kumtia hatiani mshitakiwa.

Katika mapitio yake, alibaini kuwepo na kasoro kinyume na Sheria ya Uchawi na kuamua kufuta kesi ya jinai namba 11 ya mwaka 2022.

Jaji Dk Utamwa alisema kwa mujibu wa hati ya mashitaka, Mahakama ya Wilaya ya Ludewa ilimtia hatiani Chale kwa Sheria ya Uchawi Sura namba 18, kifungu namba tatu (a) na kifungu namba tano, kifungu kidogo cha (1) cha sheria hiyo.

Alisema kwa mujibu wa hati ya mashitaka mahakama hiyo ya wilaya ilisema marejeo ya sheria hiyo yamefanywa mwaka 2022 na kusema mshitakiwa Februari Mosi mwaka 2020 akiwa katika Kijiji cha Iwela wilayani Ludewa mkoani Njombe alifanya kitendo cha jinai kinachoonesha nguvu za kichawi kwa Vediana Chale.

Alisema mapitio ya kesi hiyo yamebaini kuwepo kwa makosa ya kisheria yasiyorekebishika katika kesi namba 11, 2022 ikiwa ni pamoja na muandaaji wa hati ya mashitaka kumshitaki Chale kwa sheria isiyokuwepo.

Aidha, Jaji Dk Utamwa alisema mahakama ya Ludewa ilisema Sheria ya Uchawi imefanyiwa marekebisho mwaka 2022, kitendo ambacho si kweli kwa kuwa marejeo ya sheria hiyo ya mwisho yalifanywa mwaka 2002.

Aidha, Mahakama Kuu ilisema ushahidi uliotolewa mahakamani haujitoshelezi kumtia Chale hatiani na hata kama angefunguliwa kesi hiyo kwa sheria ya marejeo sahihi ya mwaka 2002, bado kusingekuwepo na ushahidi wa kutosha dhidi yake.

Mahakama Kuu ilieleza hakuna sehemu Chale anakiri kuwa yeye ni mchawi au anaweza kufanya vitendo vya kichawi isipokuwa kulikuwa na maelezo aliyoandika kwa mlinzi wa amani yanayomwonesha kuwa amekiri yeye ni mchawi na kuwa hata hivyo maelezo hayo yamebainika hayakukidhi vigezo.

“Utaratibu ni kuwa mtu anapokwenda kukiri uchawi aende kwa kupenda yeye na asishurutishwe au kupigwa na mkaguzi wa amani lazima aandike amefikaje hapo kwake, je, ameletwa na nani, na watu au amekuja mwenyewe na hicho anachokikiri kiwe kosa kisheria linaloweza kuthibitika mahakamani,” ilisema sehemu ya uamuzi wa Mahakama Kuu iliyotolewa na Jaji Dk Utamwa Septemba 13 mwaka huu.

Machi Mosi mwaka huu, Chale alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ludewa kwa mashitaka ya kujihusisha na uchawi kinyume na sheria ya Uchawi Sura namba 18.

Ilidaiwa mahakamani kuwa Chale alimfanyia vitendo vya kichawi mtoto wa mdogo wake aitwaye Vediana Antony Chale na kumsababishia ukichaa.

Baada ya kusikiliza ushahidi, Agosti 29 mwaka huu mahakama hiyo ilimtia hatiani kwa kutumia vifungu tajwa awali na ikamhukumu kifungo cha miaka mitano jela.

Wakili wa kampuni ya uwakili ya Vertex, Antipas Lakam alisema uamuzi wa Mahakama Kuu umedhihirisha namna ilivyo vigumu kuthibitisha tuhuma za uchawi mahakamani.

“Sheria hii ni wakati sasa iangaliwe upya ama iboreshwe kulingana na mazingira yetu au ifutwe kwa sababu sio rahisi kupeleka vielelezo pasi na shaka kuthibitisha uchawi au vitendo vya uchawi, mahakamani,” alisema Lakam.

Alisema sheria hiyo ilitungwa mwaka 1928 kwa lengo la kudhibiti watu kujihusisha na imani potofu na vitendo vya kichawi lakini ni vigumu kuvithibitisha mahakamani.

Sheria hiyo imefanyiwa mapitio mara nne yakiwemo ya mwaka 1935, 1956, 1998 na mwaka 2002.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button