Mahakama: Stella alijinyonga akiwa Mahabusu

DAR ES SALAAM: Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni, Kinondoni, Dar es Salaam imesema imeridhika kuwa kifo cha Stella Moses kilitokana na yeye mwenyewe kujinyonga akiwa mahabusu ya Kituo cha Polisi Mburahati alipokwenda kujisalimisha kutokana na ripoti ya daktari ilivyoeleza.

Uamuzi huo umetolewa leo na Hakimu Mkazi, Jackline Rugemalira chini ya Mahakama ya Korona, baada ya mleta maombi kuiomba mahakama iridhie kufanya uchunguzi wa kifo cha utata cha Stella akiwa chini ya mahabusu ya Polisi.

Stella alifariki dunia usiku wa Desemba 20, 2020, akiwa mahabusu ya Kituo cha Polisi Mburahati alikojisalimisha baada ya kupata taarifa kuwa alikuwa anahitajika huku polisi wakidai kuwa mtuhumiwa huyo alijinyonga.

Hata hivyo, wanafamilia hawakukubaliana na maelezo hayo, badala yake wakaomba ufanyike uchunguzi huru kujiridhisha chanzo cha kifo chake wakati Jeshi la Polisi likishinikiza mwili wa marehemu uzikwe.

Shauri hilo lilifunguliwa na shemeji wa marehemu, Emmanuel Kagongo kwa niaba ya familia ya marehemu dhidi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi (IJP), Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kipolisi Mburahati (OCD), Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Hakimu Rugemalira amesema mahakama inazingatia ushahidi ambao ni taarifa ya uchunguzi wa mwili wake ya Februari 25, 2020 inaonesha kifo hicho kimesababishwa na jeraha kichwani (head injury) na kufeli mfumo wa kupumua (respiratory failure).

“Kwa ushahidi wa ripoti ya daktari marehemu alikutwa na mauti kwa jeraha kichwani na kwa sababu shahidi waliomfikisha hapo hospitali walieleza kuwa marehemu alifika kituoni hapo kutokana na tuhuma zilizokuwa zinamkabili Tunduma,” amesema Hakimu.

Hakimu Rugemalira amesema kutokana na ripoti ya daktari kilichosababisha kifo ni respiratory na injury,lakini hakuna shahidi mwingine aliyeeleza kuwa jeraha lilitokana na nini, kwa hiyo Mahakama inaridhika kuwa kifo cha Stella kilitokana na yeye mwenyewe kujinyonga.

Habari Zifananazo

Back to top button