Mahakama yaahirisha uchunguzi kifo cha mahabusi

Mahakama yaahirisha uchunguzi kifo cha mahabusi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kinondoni, Kivukoni Dar es Salaam, imeahirisha kufanyika kwa uchunguzi wa chanzo cha kifo cha mfanyabiashara, Stella Moses aliyefia mahabusu ya Kituo cha Polisi Mburahati mwaka 2020 hadi itakapopitia nyaraka halisi za maelezo ya mashahidi.

Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga, baada ya kupitia hoja za pande zote mbili na maoni ya washauri wa mahakama (wazee wa baraza) kuhusu pingamizi lililowasilishwa na upande wa wadaiwa na nyaraka mpya katika shauri hilo.

“Baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote mbili na kupata maoni ya washauri wa mahakama, mahakama inaona ni busara iahirishe huu uchunguzi ili iweze kuzipitia hizo nyaraka ambazo ziliwasilishwa mahakamani,” alisema Kiswaga.

Advertisement

Pia aliagiza nyaraka hizo halisi ziwasilishwe mahakamani hapo siku ya Jumatano ya wiki ijayo (Machi 22, mwaka huu) ili mahakama iweze kuzipitia, kwa sababu nyaraka zilizokuwa zimewasilishwa zilikuwa ni nakala.

Baada ya hakimu kutoa uamuzi, wakili wa walalamikaji, Madeleka aliieleza mahakama kuwa anatoa taarifa ya mdomo ya kukata rufaa kwa sababu hawajaridhika na uamuzi huo.

“Tunaona tunapoteza muda katika mahakama hii ni bora twende mbele katika Mahakama Kuu ili wateja wangu waweze kupata haki yao leo hatukuja kuchunguza nyaraka, tulikuja kuanza kuchunguza chanzo cha kifo cha Stella,” alidai.

Awali, kabla ya pande hizo kuwasilisha hoja zao, Hakimu Kiswaga alisema shauri hilo lilipokuja Machi 9, 2023, wakili wa wajibu maombi, Job Mrema aliomba uchunguzi usiendelee na kuomba kutumia jalada jipya aliloleta, lakini wakili wa waleta maombi Madeleka alipinga.

Stella alifariki dunia usiku wa Desemba 20, 2020, akiwa mahabusu ya Kituo cha Polisi Mburahati alikojisalimisha baada ya kupata taarifa kuwa alikuwa anahitajika huku polisi wakidai kuwa mtuhumiwa huyo alijinyonga.

Hata hivyo, wanafamilia hawakukubaliana na maelezo hayo badala yake waliomba ufanyike uchunguzi huru kujiridhisha chanzo cha kifo chake wakati Jeshi la Polisi likishinikiza mwili wa marehemu uzikwe.