Mahakama yaelezwa Padri alivyonajisi mtoto akiungama

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Moshi imeelezwa namna Paroko wa Parokia Teule ya Mtakatifu Dionis Aropagita ya Jimbo Katoliki la Moshi, Padri Sosthenes Bahati (41) anavyodaiwa kumnajisi mtoto wa miaka 12 akiungama.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mwandamizi, Salome Mshasha, wakili wa serikali mwandamizi, Kassim Nasri alidai mshitakiwa alitenda kosa hilo Agosti 12 mwaka huu akiwa ofisini kwake.

Ilidaiwa mahakamani hapo kwamba siku ya tukio mtoto huyo alikwenda katika Kanisa Katoliki Mtakatifu  Dionis Aropagita lililopo eneo la Kawawa kwa lengo la kushiriki mafundisho ya kipaimara.

Wakili Nasri alidai kuwa jioni ya siku hiyo mtoto huyo alirudi kanisani hapo kuungama dhambi na alimkuta mshitakiwa akiwa amekaa katika kiti, akapiga magoti mbele ya kiongozi huyo wa kanisa ili kuungama.

Alidai wakati mtoto huyo akiungama mshitakiwa alimshika mabega na kisha kumpapasa mwilini, kifuani na sehemu za siri.

Wakili Nasri alidai kuwa baada ya kumpapasa alimuegemeza ukutani na kunyanyua sketi ya mtoto huyo na akamtaka aishikilie na kisha akamshusha nguo za ndani.

Alidai kuwa mstakiwa alipandisha kanzu na akafungua suruali, akamnajisi mtoto huyo.

Wakili Nasri alieleza mahakama kwamba mtoto alimweleza mama yake na uchunguzi ulipofanyika ilibainika mtoto huyo alinajisiwa na mshitakiwa huyo.

Mshitakiwa alikana mashitaka hayo lakini alikiri kutambuliwa katika gwaride la utambulisho mbele ya mtoto huyo.

Wakili huyo alidai upande wa mashitaka una mashahidi 10 na watatoa ushahidi mfululizo. Wakili wa utetezi, Edwin Silayo aliomba mahakama hiyo isisikilize kesi hiyo ili kumpa fursa azungumze na mteja wake kwa kuwa ni mara ya kwanza anakutana naye.

Habari Zifananazo

Back to top button