Mahakama yakataa kuendeshwa na ofisi ya DPP

Mahakama yakataa kuendeshwa na ofisi ya DPP

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Moshi mkoani Kilimanjaro imesema mahakama inaendeshwa kwa mujibu wa sheria hivyo ofisi ya Mwendesha Mashitaka (DPP) haiwezi kuiendesha.

Hakimu Mkazi Mfawidhi, Salome Mshasha alisema hayo Jumatatu akijibu hoja za upande wa utetezi wa kesi ya uhujumu uchumi namba 2 ya mwaka 2022 inayomkabili aliyewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya.

“DPP hawezi kui- ‘control’ mahakama, naye ni mlalamikaji tu kwani ndiye anayeleta mashauri mahakamani, lakini DPP anafuata miongozo katika ofisi yake, siyo sahihi kusema anaiendesha mahakama hii,” alisema Hakimu Salome.

Advertisement

Awali Wakili wa utetezi, Hellen Mahuna aliilaumu ofisi ya DPP kwa kutorekebisha hati ya mashitaka kwa kuwa iliyosomwa mahakamani hapo inawataja washtakiwa watano lakini yupo mmoja, Sabaya kwa kuwa wenzake wanne wameachiwa.

“Mheshimiwa hii inaonesha DPP, anafanya masuala vile anataka, hati iliyosomwa na wakili msomi, Sabitina Mcharo inataja washitakiwa watano licha ya wanne kuachiwa wiki iliyopita, upande wa utetezi hauna pingamizi juu ya walioachiwa,” alisema.

Wakili Hellen aliiomba mahakama ielekeze Jamhuri ikamilishe upelelezi kwa madai kuwa Sabaya ni mgonjwa lakini pia ofisi ya DPP itoe kibali ili mshitakiwa afahamu hatma yake asiendelee kuteseka gerezani.

Hakimu Salome Mshasha alikiri hati ya mashitaka inapaswa kurekebishwa na akaagiza upande wa Jamhuri uifanyie marekebisho ili imtaje mshitakiwa Lengai Ole Sabaya pekee.

Awali wakili wa Jamhuri, Sabitina Mcharo, aliieleza mahakama upelelezi wa shauri hilo haujakamilika lakini pia ofisi ya DPP haijatoa kibali kwa mahakama hiyo kusikiliza kesi hiyo.

 

 

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *