MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imekubali ombi la wanachama wawili wa chama cha NCCR -Mageuzi la kutoa amri ya zuio kwa aliyewahi kuwa Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini na wenzake wanane kuendesha vikao vilivyopangwa kufanyika Septemba 8, 9 na 10 mwaka huu.
Wanachama hao, Angelina Mutahiwa ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara na Hemedi Kanoni waliwasilisha maombi mahakamani Septemba 6 mwaka huu dhidi ya Haji Ambar Khamis, Martha Chiomba, Ameir Mshindani Ali, Susanne Masele, Beati Mpitabakana, Martin Mng’ong’o, Ramadhan Manyeko, Selasini, Hassan Ruhwanya na Bodi ya Wadhamini ya NCCR-Mageuzi (Registered Trustees Of NCCR-Mageuzi).
Jaji Edwin Kakolaki alitoa uamuzi huo jana wakati kesi hiyo iliposikilizwa kwa mara ya kwanza na upande wa wapeleka maombi kuwasilisha ombi hilo la kutaka vikao hivyo vizuiwe.
Wakili wa wapeleka maombi, Juma Nassoro alidai waliwasilisha maombi ya msingi kwa hati ya dharura kwa kuwa kulikuwa na vikao vilivyopangwa kuanza jana ndani ya chama hicho.
“Maombi yameombwa chini ya hati ya dharura, kuna vikao vinaendelea tarehe 8, 9 na tarehe 10 ambavyo vitaathiri shauri hili, tunaomba zuio kwa wajibu maombi wasiendelee na vikao hivyo mpaka maombi hayo yatakaposikilizwa na kuamriwa,” alisema Nassoro.
Hoja hiyo ilipingwa na mmoja wa wajibu maombi, Mpitabakana aliyedai kuwa kuzuiliwa kwa vikao hivyo ni kuzorotesha maendeleo ya chama.
Mjibu maombi Mng’ong’o alipinga hoja hiyo na kudai kuwa wapeleka maombi hawakueleza ni kwa namna gani vikao hivyo vitaathiri shauri hilo.
Nassoro alisema hakuna mjibu maombi yeyote aliyetoa sababu ni kwa nini vikao hivyo visizuiliwe na aliongeza kuwa yeye hajazuia vikao muhimu visiendelee kwa maendeleo ya chama bali wajibu maombi wasishiriki vikao hivyo.
“Nimeangalia hoja za pande zote mbili kuhusu maombi ya kuzuia mikutano ambapo kuna mmoja ulianza leo tarehe saba ingawa sina uhakika na mingine imesemwa inaendelea, nimeombwa nisitishe hivi vikao,” alisema Jaji Kakolaki.
Aliongeza: “Kwa kuzingatia hoja hizo mahakama ilipata fursa ya kupitia kwa haraka maelezo ya kiapo cha waleta maombi ikieleza kuwepo mpango wa kuendesha hivyo vikao. Mahakama imejiridhisha na ikajikita katika hoja ya hivi vikao vilivyobaki kama vizuiliwe au la.”
Jaji Kakolaki alitoa amri kwamba mjibu maombi wa kwanza hadi wa tisa wanazuiwa
kuratibu na kushiriki vikao vilivyopangwa kufanyika ndani ya chama hadi maombi haya yatakapotolewa uamuzi.
Watoa maombi walisimamia hoja nne, ya kwanza ikiwa ni kuiomba mahakama itoe amri ya kubatilisha Mkutano wa Halmashauri ulioratibiwa na wajibu maombi Mei 21, 2022 na yote yaliyozungumzwa na kuamuliwa.
Katika kikao hicho cha Mei 21, Selasini na wenzake walifikia uamuzi wa kumsimamisha uenyekiti wa chama hicho, James Mbatia.
Pia wapeleka maombi waliiomba mahakama itamke kuwa wajibu maombi hawana mamlaka ya kuitisha vikao vya Kamati Kuu, Halmashauri Kuu wala vikao vya Sekretarieti vya NCCR-Mageuzi.
Katika hoja ya tatu waliomba mahakama izuie vikao vilivyopangwa kufanyika Septemba 8, 9 na 10, 2022 hadi pale shauri lao la msingi litakaposikilizwa na kutolewa uamuzi na hoja ya nne waliomba amri ya zuiyo la kudumu dhidi ya Selasini na wenzake kuitisha vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Chama cha NCCR-Mageuzi.