MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi, Kisutu, imemwachia huru, Amani Philipo mkazi wa Mbezi, Dar es salaam aliyekuwa akikabiliwa na mashitaka ya kumuua kwa kukusudia, askari wa usalama barabarani, Ssajent Mensah, baada ya upande wa mashitaka kushindwa kuthibitisha mashitaka dhidi yake.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu, Lumuli Mbuya alisema wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo, upande wa mashitaka walipeleka mashahidi na vielelezo 6, ambapo katika vielezo hivyo kulikuwa na taarifa ya uchunguzi wa kifo,ramani ya tukio, maelezo ya shahidi namba 1, maelezo ya shahidi namba 3, maelezo ya shahidi namba 4 na onyo la polisi.
Alisema kwa upande wa utetezi walikuwa na mashahidi wawili, ambao ni mshitakiwa mwenyewe na shahidi Samuel Thomas, ambaye siku hiyo ya tukio walishinda wote na mshitakiwa tangu asubuhi hadi saa 4 usiku.
Mbuya alisema kuwa shahidi Samuel alidai kuwa yeye siku hiyo akiendesha gari la Spacio, walitoka Tangi Bovu saa tatu na nusu usiku, ambako walikunywa bia kidogo kisha yeye na Amani wakaondoka kwenye Baa ambayo inamilikiwa na mtu aliyemtaja kwa jina la Michael.
Alidai alimfikisha Amani kwake Mbezi Africana saa nne usiku na yeye kuelekea kwake Tegeta na kumsisitiza Amani waonane siku inayofuata kwa ajili ya kutekeleza azma yao ya kuchoma nyama.
Samuel alidai siku iliyofuata Julai 23, 2016, saa nne asubuhi alipigiwa simu na Amani na kuulizwa kama yupo nyumbani na alipomjibu kuwa yupo akamwambia yeye yupo getini anaomba amfungulie.
Alidai alipokwenda kufungua geti alishangaa kuona aliyeingia hakuwa Amani, bali askari aliyejitambulisha kwa jina la Ben Magufuli na kumuuliza mahala alikokuwa na Amani jana yake.
Alidai alimweleza safari yao iliyowafikisha Muhimbili hadi Baa na kisha kumrejesha nyumbani saa nne usiku.
Alisema askari alimtaka aseme ukweli, ili amsaidie Amani kwani ana matatizo, akamuuliza matatizo gani? Lakini hakumjibu bali akatoka naye nje ya geti ambako alimkuta Amani akiwa na kijana aliyemtaja kwa jina la Oswald Mang’ombe, huku wamefungwa pingu.
Mbuya alisema Samuel alidai alimuuliza Amani nini kinaendelea? Amani akajibu hata yeye hajui, kwani polisi walienda kumkamata tu akiwa nyumbani.
Hakimu Mbuya alisema katika ushahidi uliotolewa na mashahidi wa upande wa mashitaka, ushahidi wake ulikuwa na mapengo mengi hivyo umeshindwa kithibitisha kuwa mtuhumiwa alikuwa amehusika na kifo cha Sajenti Mensah.
Alisema kuwa kwa mujibu wa hati ya mashitaka inadaiwa kuwa mnamo Julai 22, mwaka 2016, mshitakiwa Amani Philipo majira ya saa 2 usiku, eneo la mataa ya Sayansi Dar es Saalam kwa kukusudia alimuua Sajenti Mensah kwa kumpigia risasi ya kifua upande wa kulia.