Mahakama yatoa hati za talaka 444 miezi 4

ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Alex Malasusa ameziomba mamlaka ziboreshe sheria ili kupunguza kasi ya talaka nchini.

Dk Malasusa alisema hayo juzi jioni alipotembelea Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke mkoani Dar es Salaam. “Nina hakika talaka zisizokuwa na sababu zipo nyingi sana, leo ndiyo nimeshangaa kwamba mtu anaamua hata kwenda kujiunga na dini au dhehebu nyingine ili kumfanya mwenzake amuache,” alisema Dk Malasusa.

Aidha, amehimiza Watanzania waandike wosia, na aliiomba mahakama itoe semina na mafundisho ili kuondoa dhana potofu kuhusu suala hilo.

“Sisi Waafrika kuandika wosia ni kama kujichuria au kwamba upo tayari kuondoka, kumbe ni utaratibu tu na mimi nina hakika mahakama itakuwa mahali pazuri kwenye kesi za jinai na tutawapunguzia kazi mahakimu na majaji kama Watanzania wengi tutaandika wosia,” alisema kiongozi huyo mkuu wa KKKT.

Aliongeza: “Sisi tupo tayari na mimi nitaongea na viongozi wenzangu wa dini wote, Waislamu na madhehebu ya Kikristo kuona namna gani tunaweza kuhamasisha waumini walio chini yetu wawe tayari kuandika wosia”. Ziara ya Dk Malasusa katika kituo hicho ni matokeo ya juhudi zilizofanywa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma alipokwenda kufungua Kituo cha Msaada wa Kisheria katika Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam.

Katika ziara hiyo, Dk Malasusa alifuatana na wachungaji na wakuu wa majimbo wa kanda za kanisa hilo takribani 31. Jaji Mfawidhi wa kituo hicho, Mwanabaraka Mnyukwa alisema Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 Sura ya 29 inatambua ndoa zilizofungwa katika taasisi za dini na pia mahakama inazingatia imani ya marehemu katika kushughulikia mirathi.

Jaji Mfawidhi Mnyukwa alisema masuala ya mirathi na ndoa yana uhusiano na imani hivyo ushiriki wa viongozi wa dini hauepukiki katika kushughulikia mashauri hayo mahakamani.

“Kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Aprili 2024, kituo kilitoa jumla ya hati za talaka 444. Idadi hii inadhihirisha wazi kuwa viongozi wa dini mnalo jukumu kubwa katika kuisaidia jamii katika eneo hili,” alisema Jaji Mfawidhi Mnyukwa.

Jaji Mfawidhi Mnyukwa aliwaeleza viongozi hao kuwa mahakama hukosa mamlaka ya kusikiliza shauri la mirathi inapokosekana fomu namba tatu ambayo inatolewa na Bodi za Usuluhishi wa Migogoro ya Ndoa zilizoundwa na taasisi za serikali na dini.

Alisema pia mahakama huamua sheria ipi itumike katika shauri la mirathi kwa kuzingatia imani ya dini ya marehemu, hivyo hayo yote yanaonesha nafasi kubwa waliyonayo viongozi wa dini katika usikilizaji wa mashauri ya mirathi na ndoa mahakamani.

Habari Zifananazo

Back to top button