Mahakama yaweka mikakati mipya kuepuka makosa ya kiufundi

MOROGORO: MAHAKAMA Kuu ya Tanzania imeweka  jitihada kubwa katika kuhakikisha Majaji  na Mahakimu nchini  wanaondokana na makosa ya kiufundi  yanayosababisha majangili kuachiwa hata pale wanapokutwa wamefanya makosa kwa kutoa  adhabu isiyostahili.

Hayo yameelezwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mustapher Siyani  mjini Morogoro kupitia  hotuba  yake iliyosomwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro, Latifa Mansoor.

Jaji Mfawidhi Mansoor alimwakilisha Jaji Kiongozi  kufungua  mafunzo ya siku tano yaliyoanza  ya uendeshaji mashauri ya makosa ya Wanyamapori na Maliasili  yanayofadhiliwa na  Shirika lisilo la Kiserikali la Pams Foundation kwa kushirikiana na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA).

Mafunzo hayo yanawashirikisha washiriki 157 ambao ni Majaji, Maofisa wa Mahakama, Waendesha mashitaka  pamoja na Wapelelezi.

Alisema ,Mahakama imekuwa ikiwashughulikia majangili wakiwemo wa meno ya tembo na nyaraka za Serikali ambao hufikishwa mahakamani na kuhukumiwa,  kifungo chake huwa ni miaka 20 na fidia kwa serikali.

Amesema kuna  baadhi ya kesi ambazo hazijapelelezwa ipasavyo na kuwafanya majangili kutoka kwa ajili tu kuna makosa ya kiufundi katika upelelezi , hivyo  mafunzo  hayo yanalenga  kuondokana na makosa ya kiufundi na  kuhakikisha majangili wanapata adhabu inayostahili.

Hivyo amesema majangili wanapojitajirisha kupitia wanyamapori na misitu kiharamu wasiposhughulikiwa , faida wanazozipata zinatumika katika vitu vingi  haramu ikiwemo kufanya ugaidi na kuwezesha vitu vingi haramu duniani.

Pamoja na hayo amesema, zipo  juhudi zinafanywa na Shirika la Uhifadhi Tanzania (TANAPA) pamoja na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kuhifadhi aina za wanyamapori waliopo  kwenye hatari ya kupotoweka  ikiwemo Nyati.

Naye Mkurugenzi wa Mafunzo wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto , Dk Patricia Kisinda amesema ,tangu kuanzishwa kwa mafunzo hayo jumla ya maofisa wa mashitaka, mahakama  na wadau  wengine 250 wamepatiwa.

“ Tumeanza na Mikoa mitano ya Morogoro, Mtwara, Lindi, Dar es Salaam na Pwani na lengo letu ni kuwafikia  walengwa 757 kwa mwaka huu (2023)” amesema Dk Kisinda.

 

Habari Zifananazo

Back to top button