MAHOJIANO MAALUMU… Bosi Ikulu afunguka makubwa

KATIBU Mkuu Kiongozi wa zamani, Balozi Dk Matern Lumbanga

KATIBU Mkuu Kiongozi wa zamani, Balozi Dk Matern Lumbanga (76) amesema wakati akiwa mtumishi wa umma hakukubali kuonewa, kuonea wengine au kudharauliwa.

Kiongozi huyo kutoka jamii ya wakulima na wavuvi Mlimba mkoani Morogoro anasema hakukubali kuyumbishwa na alikuwa na msimamo kwa aliyoyaamini.

Balozi Lumbanga alisema hayo nyumbani kwake Masaki, Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) na akasema alikuwa Katibu Mkuu Kiongozi kwa miaka 11.

Advertisement

Kupinga uteuzi

Dk Lumbanga alisema wakati akiwa mtumishi hakukubali kukiuka sheria na ametoa mfano kuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, Dk John Magufuli alimteua awe Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA) kwa kipindi cha tatu lakini alipinga.

Alisema alimweleza Dk Magufuli kuwa sheria inaeleza kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya PPRA atakuwa kwenye nafasi hiyo kwa vipindi viwili vya miaka mitano mitano hivyo haikuwa sahihi kumteua yeye aendelee kwa kipindi cha tatu.

Balozi Lumbanga alisema Dk Magufuli alimweleza kuwa hakukosea kumteua kwa sababu aliamini kuwa yeye (Dk Lumbanga) ndiye alikuwa anafaa kuendelea na jukumu hilo.

Alisema kwa kuwa Rais Magufuli alikuwa ameshaamua hivyo ilibidi aendelee na jukumu hilo hadi Februari mwaka huu.

Kujiamini

Dk Lumbanga alisema hakuogopa kusema ukweli hata kwa mabosi wake wakiwamo marais.

Alitoa mfano kuwa aliwahi kumweleza Rais Ali Hassan Mwinyi kuwa ingawa yeye ni kiongozi wa nchi lakini alikuwa na mipaka ya madaraka yake.

Alisema baadhi ya waziri na viongozi wengine waliona kuwa hakuwa na nidhamu kumkosoa Rais Mwinyi lakini yeye aliona ulikuwa ni wajibu kusema alichoona kilikuwa sahihi.

“Mimi siogopi mtu, kwenye ukweli nitasema, kama litani-cost let it be (kama litanigharimu acha iwe hivyo) lakini mwenye akili atajua, atakayekuwa mvumilivu utamchukua, utamchukua itafika mahala mtaelewana,” alisema Balozi Lumbanga.

Alisema kiongozi hatakiwi kuwa mwoga na akiwa hivyo haisaidii nchi.

“Halafu unakuwa wa kwanza kulalamika ooh nchi inaharibiwa, wewe huoni kama na wewe umechangia katika kuiharibu nchi. Yaani unaogopa kusema jambo ambalo unajua hili si sawa, liseme,” alisema Dk Lumbanga.

Ukweli kwa Nyerere

“Mimi nilikuwa siogopi kumwambia mtu ukweli, hata Nyerere (Baba wa Taifa, Julius Kambarage) siku nyingine aliniita yupo pale Msasani nikwambia hili Rais ukiniagiza nitalipokea lakini nakwambia sitatekeleza,” alisema.

Alisema alimpa ufafanuzi Baba wa Taifa kwa nini alisema vile na Nyerere akamuita msaidizi wake akamweleza kwamba Lumbanga alikuwa na akili sana.

Alimuudhi Sokoine

Dk Lumbanga alisema mwaka 1976 Waziri Mkuu wakati huo, Edward Sokoine alimweleza kuwa alikuwa amekubaliana na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Nyerere kwamba serikali ipeleke mameneja wa mipango vijijini ili kuharakisha maendeleo.

Alisema wakati huo yeye alikuwa Kamishna wa Mipango katika ofisi ya Waziri Mkuu na alimweleza Sokoine kuwa hakukubaliana na jambo alilomweleza.

Dk Lumbanga alisema walimshauri Sokoine kwamba wasifanye mabadiliko ya ghafla, wangeanza na mikoa miwili au mitatu na pia alimuuliza kiongozi huyo kwamba meneja wa kijiji angefanya kazi gani.

Alisema msimamo wake ulimuudhi Sokoine na yeye (Dk Lumbanga) na wakuu wa idara wanne ndani ya mwezi walihamishwa na yeye alihamishiwa kuwa Mkurugenzi wa Mipango katika Wizara ya Maliasili na Utalii.

Dk Lumbanga alisema uhamisho huo lilikuwa jambo kubwa na hata wabunge waliihoji serikali ni kwa nini wakuu wa idara tano katika ofisi ya Waziri Mkuu wamehamishwa.

Alisema mwaka mmoja baadaye serikali ilisitisha utekelezaji wa uamuzi wake na Sokoine aliomba radhi bungeni.

Apinga kupunguzwa mshahara

Dk Lumbanga alisema wakati akiwa Kamishna wa Mipango ofisi ya Waziri Mkuu mshahara wake ulikuwa MS 12 na alipohamishiwa kuwa Mkurugenzi wa Mipango Wizara ya Maliasili na Utalii mshahara wake ulipunguzwa hadi MS 10.

Alisema jambo hilo lilimsononesha, aliandika barua kwa Katibu wa Wizara hiyo, Julius Sepeku kupinga jambo hilo.

Dk Lumbanga alisema Sepeku alimwita akamweleza kuwa alikuwa ametumia lugha ambazo hazikustahili kutumiwa na mtumishi kumwandikia kiongozi wake.

Alisema alimjibu Sepeku kwamba yeye alikuwa ameandika na iende hivyo na kama alitaka kurekebisha arekebishe yeye.

Balozi Lumbanga alisema Sepeku aliirekebisha barua hiyo, akamuita akampa aisome kama ipo sawa, ilikuwa sawa na yeye (Dk Lumbanga) akaisaini ili ikafanyiwe kazi.

Aeleza alivyomkasirikia Mongella

Dk Lumbanga alisema siku moja Waziri wa Maliasili na Utalii wakati huo, Getrude Mongella alimweleza waende Ikulu, Dar es Salaam kumuona Rais Ali Hassan Mwinyi.

Alisema walipofika huko bosi wake alimweleza Rais Mwinyi kuwa ni yeye (Dk Lumbanga) alikuwa na uzoefu kwenye wizara hiyo hivyo akahoji ni kwa nini mamlaka zilikuwa hazimpandishi cheo.

Dk Lumbanga alisema kauli ya Mongella ilimuudhi kwa kuwa aliona kama bosi wake alimpeleka Ikulu ili akaombe cheo hivyo aliondoka hapo akiwa amekasirika.

Alisema alirudi ofisini akamweleza katibu muhtasi wake kuwa Waziri akirudi amjulishe. Dk Lumbanga alisema muda mfupi baadaye Mongella alikwenda ofisini kwake (Lumbanga) akamweleza kuwa alibaini alikuwa amekasirika.

Kwa mujibu wa Dk Lumbanga, hadi wakati huo, alikuwa amefanya kazi wizarani hapo na mawaziri wanane na makatibu wakuu wanane ndani ya miaka 10.

Alisema baada ya wiki mbili, alipewa taarifa kuwa alikuwa ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii.

Dk Lumbanga alisema siku chache baadaye alielezwa kulikuwa na mabadiliko kwa kuwa wizara hiyo iliunganishwa na Wizara ya Ardhi hivyo yeye alipangiwa kuwa Naibu Katibu Mkuu anayesimamia maliasili na Abdul Mshangama angesimamia sekta ya ardhi.

Alisema alimweleza Mshangama kuwa alikuwa na msimamo kwamba kwenye kosa asingemficha na baada ya mwaka alipandishwa kuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo.

Katika takribani saa 2:50 za kuzungumza naye Lumbanga alionesha kuwa yeye ni muwazi na alisimulia namna alivyopata magari aliyoyaegesha nyumbani kwake.

Alisema gari mojawapo Toyota RAV 4 ni la mkewe, lingine alipewa na Idara ya Usalama wa Taifa kuthamini mchango wake katika kazi zao.

Dk Lumbanga alisema alipewa gari hilo wakati anaondoka kwenda kufanya kazi Geneva, Uswisi. Alisema gari lingine alinunuliwa na serikali baada ya kurudi kutoka Geneva.

Darasa la kwanza wiki mbili

Alisema wakati anakua, alipenda kusoma masuala ya uchumi na takwimu na alikuwa na ndoto za kufanya kazi kwenye mashirika ya umoja wa mataifa.

Dk Lumbanga alisema alikuwa katika mazingira magumu kwa kuwa baba yake mzazi aliaga dunia wakati hajaanza hata shule.

Alisema kutokana na uwezo wake mkubwa darasani alisoma darasa la kwanza kwa wiki mbili tu na kote alipokwenda alikuwa akiongoza kwenye mitihani.

Balozi Lumbanga alisoma katika Shule ya Msingi Mkungumero, Mlimba, baadaye alisoma masomo ya juu ya elimu ya msingi katika shule ya Igota iliyopo Mahenge zote za mkoani Morogoro.

Alisoma masomo ya sekondari katika Shule ya Sekondari ya Kwiro iliyopo Mahenge na baadaye akasoma masomo ya sanaa katika Shule ya Sekondari ya Pugu, Dar es Salaam.

Dk Lumbanga ni mchumi, ana Shahada ya kwanza ya Uchumi aliyoipata katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Pia ana shahada ya uzamili na shahada ya uzamivu katika uhusiano wa kimataifa kuhusu masuala ya umasikini aliyoipata Shule ya Diplomasia na Uhusiano wa Kimataifa ya Uswisi.

Balozi Lumbanga ameitumikia Serikali ya Tanzania tangu mwaka 1972 katika nafasi mbalimbali, amestaafu utumishi wa umma Julai mwaka jana.

Amewahi kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Maliasili na Utalii (1989-1990), Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi (1990-1991), Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara (1991-1992) na Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi (1992-1995).

Mwaka 1995 aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu Kiongozi nafasi aliyoishika hadi mwaka 2006 alipoteuliwa kuwa Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika ofisi za Umoja wa Mataifa (UN) nchini Uswisi.

Kiongozi huyo ni baba wa watoto watano aliowazaa na mkewe, Ethel Lumbanga akiwamo Mordigard, Herieth, Emmanuel, Clara na Catherine.

Alikutana na Ethel wakati wote wanafanya kazi ofisi ya Waziri Mkuu yeye akiwa Kamishna wa Mipango na mwenza wake akiwa Mhasibu na walifunga ndoa mwaka 1976.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *