Majaji, mahakimu wataka kesi baada ya upelelezi

MAJAJI na mahakimu waliowahi kufanya kazi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wamependekeza mbele ya Tume ya Kuangalia Haki Jinai nchini kuondolewa kwa utaratibu wa kuwafikisha watuhumiwa mahakamani kabla ya upelelezi kukamilika.

Aidha, imependekeza kesi za uhujumu uchumi zipelekwe moja kwa moja Mahakama Kuu badala ya kupelekwa mahakama za wilaya au za hakimu mkazi ambazo hazina mamlaka ya kuzisikiliza.

Jaji wa Mahakama Kuu, Augustine Rwizile alisema Dar es Salaam jana kuwa wamependekeza sheria mbalimbali ikiwamo ya Makosa ya Jinai (CPA) namba 20 na Sheria ya Uhujumu Uchumi, zifanyiwe maboresho na baadhi ya taratibu zilizowekwa ambazo zinakwamisha utoaji wa haki ziondolewe.

“Mtu anashitakiwa kwa kosa la mauaji, mahakama tunasema mkamateni, peleleza mleteni wakati upelelezi umekamilika, ili siku kesi yake itakapofikishwa mahakamani tuanze kuisikiliza,” alisema Jaji Rwizile wa Kituo Jumuishi cha masuala ya familia, Temeke.

Aliwaeleza waandishi wa habari kuwa utaratibu wa kukamata watuhumiwa na kuwafikisha mahakamani kabla ya upelelezi kukamilika uondolewe na sheria iweke ukomo wa upelelezi wa kesi hizo.

Jaji Rwizile alisema kesi nyingi za uhujumu uchumi zinazopelekwa kwenye Mahakama za Wilaya na Hakimu Mkazi, zinahitaji kibali cha Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) cha kusikiliza kesi hizo, hivyo mara nyingi washitakiwa wanakaa muda mrefu bila kusikilizwa kwa kuwa mahakama hizo hazina mamlaka ya kisheria ya kusikiliza kesi.

“Suala la commital procedures linatukwaza, kuna watu wanashitakiwa kwa makosa ya uhujumu uchumi, anakamatwa kesi yake inapelekwa mahakamani tena kwenye mahakama isiyo na mamlaka ya kusikiliza, inakaa hapo huku wakipeleleza mpaka watakaposema sasa upelelezi umekamilika, tuipeleke kusikilizwa Mahakama Kuu, hii si sawa,” alisema.

Jaji Rwizile pia alisema wamependekeza sheria iweke ukomo wa upelelezi na endapo utakiukwa, mahakama itoe maamuzi ikiwemo kufuta kesi.

Alisema kutokuwepo kwa ukomo wa upelelezi kunatoa mwanya kwa waendesha mashitaka kukaa na majalada hata kwa miaka 10.

Habari Zifananazo

Back to top button