Majaliwa aagiza ujenzi ukamilike Desemba 31

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmshauri ya Wilaya ya Nkasi, William Mwakalambile ahakikishe ujenzi wa miundombinu ya Shule ya Sekondari ya Paramawe unakamilika ifikapo Desemba 31, mwaka huu.

Ni kwa kufanya hivyo amesem wanafunzi wote waliofaulu mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi watajiunga na kidato cha kwanza Januari mwakani.

Aidha, amemuagiza Mwakalambile ahakikishe anatumia fedha za makusanyo ya ndani kukamilisha mradi huo pia kutenga zaidi ya Sh milioni 100 zitumike kujenga bweni la wasichana shuleni hapo.

Majaliwa pamoja na maelekezo hayo, pia alieleza kutoridhishwa na jinsi Sh milioni 470 zilivyokwisha bila ujenzi wa mradi huo kukamilika licha ya halmashauri hiyo kuongeza zaidi ya Sh milioni 30.

“Kiasi hiki cha shilingi milioni 500 kujenga vyumba vinane vya madarasa ni kikubwa kwani Halmashauri ya Mpimbwe mkoani Katavi imetumia Sh milioni 250 kujenga vyumba 13 vya madarasa kwa viwango, hii haikubaliki,” alisema.

Majaliwa ameanza ziara ya kikazi katika Mkoa wa Rukwa ambapo ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Paramawe na Hospitali ya Wilaya iliyopo wilayani Nkasi.

Katika Shule ya Sekondari Paramawe kunajengwa vyumba vinane vya madarasa, maabara, maktaba na matundu ya vyoo ambapo alisema vimejengwa chini ya viwango.

Akizungumza baada ya kukagua ujenzi huo, Waziri Mkuu alimwagiza Katibu Tawala wa Mkoa huo kumsimamia Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi ili ahakikishe anakamilisha maeneo ya ujenzi wa shule hiyo kwa kutumia mapato ya ndani.

“Milioni 470 zimetumika na mmetumia zingine za halmashauri lakini miundombinu bado. Nataka shule hii ikamilike na Januari 2023 wanafunzi waingie,” aliagiza.

Kuhusu ujenzi wa Hospitali ya Wilaya Nkasi, Waziri Mkuu aliwaeleza wananchi kuwa serikali itaendelea kukamilisha miradi yote ya afya ikiwemo kuhakikisha vifaa tiba vinapatikana kwa ajili ya wananchi kupata huduma.

Aidha, Waziri Mkuu alimwagiza Naibu Katibu Mkuu Tamisemi -Afya kukutana na uongozi wa Halmshauri ya Nkasi ili kujua kwa nini miradi ya ujenzi wa majengo saba ya hospitali ya wilaya haujaanza wakati tayari fedha zilikwishatolewa na serikali.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Queen Sendiga alisema mkoa unaendelea na usimamizi wa shughuli za maendeleo na kuwa wananchi watapata huduma stahiki.

Habari Zifananazo

Back to top button