Majaliwa aita mjadala eneo huru la biashara Afrika

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema makubaliano ya eneo huru la biashara Afrika yana lengo la kuleta mageuzi ya kiuchumi barani humo hivyo inahitajika mikakati ili kuzitumia fursa zilizopo.

Majaliwa amesema makubaliano haya yameleta pamoja nchi 54 za Afrika na kuunda soko moja la watu takribani bilioni 1.4. Waziri Mkuu ameyasema hayo jana jijini hapa akifungua mkutano wa kimataifa wa wakuu wa mamlaka za bima barani Afrika unaohudhuriwa na wajumbe zaidi ya 200.

“Hii ni fursa kubwa ambayo inapaswa kujadiliwa kwa undani na kuwekewa mikakati kwenye mkutano huu. Ninaomba nitoe rai kwamba mkutano huu ujadili na kuweka mikakati ya namna ya kuzifikia na kuzitumia fursa zilizopo kwenye Eneo Huru la Biashara ya barani Afrika kwa ajili ya maendeleo ya Bara la Afrika na watu wake,” alisema Majaliwa.

Aliongeza: “Wataalamu wanakadiria kwamba iwapo tutaendeleza ushirikiano huu kwa kufanya biashara huru miongoni mwetu, bila shaka pato la Bara la Afrika litakua kwa wastani wa asilimia sita hadi kufikia takribani dola trilioni 66.4 kwa miaka 50 ijayo.”

Alisema Bara la Afrika lina rasilimali nyingi ikiwemo ardhi ya kilimo, mafuta, misitu, madini, mifugo na kwamba lina rasilimaliwatu ya wakazi bilioni 1.4 ambayo ni sawa na asilimia 18.2 ya watu wote duniani. Kuhusu bima alizitaka mamlaka na taasisi zinazohusika na usimamizi wa bima na hifadhi ya jamii Afrika zitoe elimu ya kutosha kwa jamii ili watu wengi wajiunge na huduma hizo.

“Mamlaka na taasisi zetu zinazohusika na usimamizi wa bima na hifadhi ya jamii ongezeni juhudi ya utoaji wa elimu ya bima na hifadhi ya jamii barani Afrika kwa namna ile ambayo nchi husika itaona inafaa,” alisema.

Alisema ni vigumu kutenganisha umuhimu wa bima na hifadhi ya jamii kwa sababu vyote vinajaribu kumlinda mtu na jamii dhidi ya majanga yanayoweza kutokea wakati wowote.

Aliwataka wataalamu hao waangalie namna ya kuifanya mifumo ya hifadhi ya jamii na pensheni iwe shirikishi kwa watu wote na hasa kuwapa kipaumbele wanawake, vijana, wazee na wakulima ambao wako katika mazingira magumu.

Habari Zifananazo

Back to top button