Majaliwa akaribisha wawekezaji sekta ya madini

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Kassim Majaliwa amekutana na ujumbe kutoka Korea Kusini uliojumuisha viongozi wa makampuni makubwa ya madini yanayohusika na mnyororo wa thamani wa uzalishaji betri za magari ya Posco Holdings, Posco International,SK, Korea Zinc  na LX International kupitia madini ya kimkakati(_critical minerals_).
Waziri Mkuu Majaliwa amewaeleza wawekezaji hao juu ya utayari wa serikali katika kushirikiana nao katika uwekezaji wao kwa kuweka mazingira mazuri ya kisera na kuboresha miundombinu canya usafirishaji kwa njia ya barabara,maji,reli na anga.
Aidha, Majaliwa amepongeza hatua iliyofikiwa kwa kampuni tatu za Faru  Graphite Corporation, Black Rock Mining Limited,  na Posco International ya Korea Kusini, kusaini hati ya makubaliano (Memorandum of Understanding – MoU) kwa ajili ya mashirikiano ya kibiashara yatakayowezesha kampuni ya Posco kupata madini ya kinywe  kutoka mradi wa kinywe wa Mahenge,Morogoro.
Akitoa maelezo ya awali,Waziri wa Madini Anthony Mavunde,  amesema ushirikiano wa Korea Kusini na Tanzania katika eneo hilo la madini ya kimkakati litasaidia kuchochea ukuaji wa sekta ya madini na kuongeza mchango wa sekta ya madini katika pato la Taifa.
Amesema, pia katika mazungumzo ya awali wameafikiana kubadilishana uzoefu wa kitaalamu pamoja na umuhimu wa kuongeza thamani ya madini hayo hapa hapa chini ili kuongeza tija na kuchochea uchumi wa ndani sambamba na upatikanaji wa ajira za kutosha kwa watanzania.
Kwa upande wa Mkuu wa Msafara wa Wawekezaji kutoka Korea Kusini  Yoon Sang Jick, Waziri Mstaafu wa Biashara, Viwanda na Nishati na Mjumbe Maalum wa Rais amesema ni dhamira ya Korea Kusini kuhakikisha inashirikiana na Tanzania katika eneo hilo  la madini mkakati na ndio sababu ameongozana na Kampuni kubwa za Madini na zenye uwezo mkubwa wa Mtaji.
Amesema,   anaamini kupitia ushirikiano huo  milango iliyofunguliwa na serikali ya Tanzania wapo tayari kuleta uwekezaji mkubwa kwenye sekta hiyo ya madini na kusaidia kuikuza.
Akitoa maelezo ya awali Balozi wa Tanzania nchini Korea Kusini Balozi Togolan Mavula amesema ni fursa ya kipekee ya nchi ya Tanzania kulitumia vizuri soko la Korea Kusini kwa madini ya kimkakati na kwamba ubalozi wa Tanzania utaendelea kuratibu upatikanaji wa wawekezaji wengi zaidi katika maeneo mbalimbali ya sekta ya madini.

Habari Zifananazo

Back to top button