WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, ametoa maagizo mbalimbali kwa Mamlaka za Maji na Mabonde, huku akikemea tabia ya mikoa na wilaya kutunishiana misuli katika kutekeleza miradi ya maji kwa wananchi.
Majaliwa ameyasema hayo leo Machi 16,2023, wakati akizindua mradi wa ujenzi wa mfumo wa usamabazaji maji kutoka matenki ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) yaliyopo Chuo Kikuu cha Ardhi hadi Bagamoyo wenye thamani ya Sh 71bilioni, unaotekelezwa na serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia.
Akikemea tabia ya viongozi wa mikoa na wilaya kutunishiana misuli, Majaliwa amesema serikali imenunua mitambo mikubwa ya kisasa 25 ya uchimbaji visima na seti tatu ya mitambo ya kujenga mabwawa, ikiwa ni mkakati wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi yanayochangia kupungua kwa maji, ikiwa ni utekekezaji wa Ilani ya CCM ya kufikisha huduma ya maji kwa asilimia 85 vijijini na asilimia 95 mijini.
“Nilikua Kigoma nimekuta eti Ruwasa Mkoa hawawapi Ruwasa wilaya mitambo kuchimba visima kisa hawana pesa za kulipa, naagiza tabia hii ife mara moja, serikali kwa serikali mnanyima nini? ” Amehoji na kuongeza:
” Toeni huduma kwa wananchi mtajua wenyewe mnavyolipana, sio mnakaa kugombana gombana, jambo hilo naagiza kwa mamlaka zote za mikoa na wilaya lisije likajirudia,” amesisitiza.
Pia amesema vyanzo vya maji vipo vingi, maji yapo ya kutosha ni marufuku umeme kukatika kwa kisingizio cha uhaba wa maji kusukuma mitambo.
Majaliwa pia ametoa siku 14 kwa wananchi ambao wapo ndani ya mradi wa ujenzi wa mfumo wa usamabazaji maji kutoka matenki ya Dawasa yaliyopo Chuo Kikuu Cha Ardhi hadi Bagamoyo wawe wameunganishiwa huduma ya maji.
“Mabomba yapo, pesa ipo, unganisheni mabomba yaende kwa wananchi, ndio maelekezo yangu kwa leo, “amesema.
Pia ameitaka Dawasa kutoa bei elekezi ya uunganishwaji maji kuepuka vitendo vya rushwa vinavyofanywa na wananchi wasio waaminifu.
” Mwananchi usikubali mtu yeyote kutoa rushwa eti uunganishwe huduma ya maji mripoti mara moja, na atakaebainika tutamshughulikia, mfumo wa malipo ya serikali unajulikana mlipe kwa ‘control number’
“Nakuagiza Mheshimiwa Aweso (Waziri wa Maji)wasimamie Mameneja wa Maji kutekeleza majukumu kwa weledi,” amesema.
Pia Majaliwa pia amekemea tabia ya watendaji wa Mamlaka za Maji kubambikia bili za maji wananchi.
“Kilio cha wananchi ni kubambikiwa bili za maji, wananchi msikubali kulipa bili kubwa kama mnaviwanda wakati maji mnatumia kwa matumizi ya kawaida nyumbani, Mamlaka za Maji nchi nzima mita zenu zioneshe kwa uwazi, msijaribu kuiharibia serikali, mnabambika bili ili wananchi waichukie serikali yao, tukikugundua tutakushughulikia, “amesema Majaliwa.
Aidha, ameagiza Wakurugenzi wote wamabonde kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili vyanzo vya maji visiharibiwe.
“Kila mmoja wetu ana wajibu wa kutunza mazingira, anayeharibu ni muhujumu uchumi, atatuua huyu, tusimchekee lazima achukuliwe hatua, utunzaji mazingira ni muhimu kila Mtanzania azingatie hili, ” amesema.
Kwa upande wake Waziri wa Maji Jumaa Aweso ameahidi kusimamia maagizo ya serikali, huku akiiomba serikali kuangalia namna ya kupunguza gharama za vifaa vinavyotumika kuunganisha maji, ili kuwawezesha wananchi wote kupata huduma hiyo.
“Niombe kwako Waziri Mkuu pamoja na jitihada za serikali kuhakikisha maji mengi yanapatikana ni muhimu sasa kuangalia bei za vifaa vya kuunganishia maji, ikiwemo mabomba bei ipunguzwe kuwezesha wananchi wote kupata maji,” amesema.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji,Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema mradi huo unathamani ya Sh bilioni 71, utasaidua kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji kwa Mkoa wa Pwani na Dar es Salaam.
“Maji kwa sasa ni mengi tuna lita za ujazo bilioni 26 na hadi sasa tumefikia asilimia 95 ya kuwafikishia huduma wateja,” amesema.
Mradi huo unalenga kuboresha huduma ya upatikanaji maji kwa wakazi zaidi ya 60,000 waliopo kati ya Kata ya Makongo jijini Dar es Salaam hadi Bagamoyo mjini mkoani Pwani, ambapo hadi sasa wateja wapya 19,000 wameshaunganishwa.
Mradi huo umehusisha ujenzi wa matenki matatu makubwa ya kuhifadhi maji yenye ujazo wa lita milioni 5 kila moja yaliyojengwa maeneo ya Vikawe, Mbweni na Tegeta A.
Mradi huu kwa wilaya ya Kinondoni utanufaisha maeneo Changanyikeni, Vikawe, Goba, Mivumoni, Mbweni, Madale, Tegeta A, Bunju, Wazo, Ocean Bay na Salasala.
kwa upande wa Bagamoyo utahudumia wakazi wa Kata ya Mataya, Sanzale, Migude, Ukuni, Mtambani, Nianjema, Kimarang’,ombe, Kisutu na Block P.
Kwa upande wa Vikawe utahudumia Kata ya Mapinga, Kwa Matumbi na Vikawe bondeni.
Kwa Mabwepande mradi unahudumia Kata ya Bunju B, Mabwepande, Mbopo wakati Kata ya Salasala mradi unahudumia Kinzudi, Mbezi, Goba na Kilongawima.