WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameondoka nchini kwenda Tunisia kumwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika mkutano wa nane wa wakuu wa nchi na serikali wa TICAD.
Taarifa ya ofisi ya Waziri Mkuu ilieleza jana kuwa mkutano huo utakaofanyika Agosti 27 na 28 mwaka huu utatoa fursa ya kupanga mikakati ya ushirikiano na ajenda za kimaendeleo zitakazotekelezwa kati ya Japan na Afrika.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Tanzania imekuwa ikishiriki mikutano hiyo tangu kuanzishwa kwake mwaka 1993.
Kufuatia uhusiano mzuri kati ya Tanzania na Japan hasa kupitia Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA), Tanzania imekuwa ikinufaika na utekelezaji wa miradi mbalimbali katika sekta za miundombinu ya barabara, nishati ya umeme, maji, elimu, afya na kilimo.
Kwa upande wa Afrika, mkutano huo unafanyika kwa mara ya pili baada ya ule wa mwaka 2016 uliofanyika jijini Nairobi, Kenya.