WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema uwekezaji una faida na kwamba suala hilo siyo kitu kipya. Alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na mamia ya wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara kwenye Uwanja vya Bandari, mjini Mtwara.
“Uwekezaji una faida, hata hapa mbele yetu (jirani na eneo la mkutano) kuna eneo la bandari limekodishwa na mtu ameweka uzio. Hawa watu wanakodisha maeneo na wanayalipia,” alisema.
Alisema mwekezaji wa kwanza kwenye Bandari ya Dar es Salaam ambako uwekezaji unapigiwa kelele, mkataba wake ulikuwa na vipengele vyenye mapungufu, vikaboreshwa mwaka 2017 na akaongezewa miaka mitano.
Majaliwa akifafanua kuhusu makubaliano baina ya serikali ya Tanzania na Dubai kupitia kampuni ya DP World alisema, “mmesema mkataba uzingatie maslahi ya Taifa, tutahakikisha mkataba huo unazingatia maslahi ya Taifa. Mmekuwa na hofu na ajira, hakuna atakayepoteza ajira. Mmekuwa na hofu na ardhi, kwamba anayekuja atachukua ardhi, siyo kweli.
Hakuna mwekezaji aliyepewa ardhi kwa sababu hata kwenye sheria za uwekezaji, mwekezaji hapewi ardhi bali anapata kibali cha kukaa juu ya ardhi na analipa kodi.
” Alisema kampuni ya DP World imewekeza kwenye nchi nyingi duniani na imejenga bandari kavu nchini Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
“Mwekezaji huyu anahudumia bandari zaidi ya 168 duniani, ana meli zaidi ya 400. Meli hizi zitaleta mizigo kwenye bandari yetu.
Ninawaomba Watanzania tumwamini Rais wetu, ana nia njema sana ya kiuchumi ya kufungua milango,” alisema.
Mapema Majaliwa alitembelea Bandari ya Mtwara na kukagua utendaji kazi wake ikiwemo gati mpya. Akiwa bandarini hapo, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Atupele Mwakibete alimweleza Waziri Mkuu kwamba ujenzi wa gati mpya yenye urefu wa mita 300 umekamilika.
Naye Kaimu Meneja wa Bandari ya Mtwara, Norbert Kalembwe alisema bandari hiyo imenunua mashine mpya ya kupakua makontena kwenye meli kwa thamani ya Sh bilioni 90. Wakati huo huo, Majaliwa alisema wanaomiliki vituo vya mafuta Mtwara, Lindi na Ruvuma wanunue mafuta hayo kutoka Mtwara ili kuongeza kasi ya uchumi kwenye bandari hiyo.
“Wanaomiliki vituo vya mafuta kwenye mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma hawana sababu ya kwenda Dar es Salaam kuchukua mafuta. Waje wachukulie Mtwara ili bandari yetu na yenyewe iwe inaleta meli za mafuta. Tusipofanya hivyo, tunaifanya bandari yetu isifanye kazi.
Kama nilivyoagiza Tanga, Waziri mwenye dhamana akae na waliojenga matenki kwenye bandari ya Mtwara ili kuweka utaratibu ambao utawawezesha kufanya biashara.
Hii itaongeza mzunguko wa fedha kwa wana-Mtwara,” alisema.