Majaliwa aonya wizi fedha za miradi

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameagiza wasimamizi wa miradi wakiwamo wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wazingatie maslahi ya taifa kwa kudhibiti matumizi ya fedha za miradi.

Majaliwa alisema hayo wakati akifungua vituo vya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji vya Nzuguni na Chamwino mkoani Dodoma ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Vituo hivyo vimegharimu zaidi ya Sh bilioni 2.3. Majaliwa alisema fedha za miradi lazima zitumike kwa madhumuni yaliyopangwa na kuangalia namna ya kupunguza gharama kwa kutumia mfumo wa wataalamu wa ndani (force account).

Alisema zimebainika dosari katika ujenzi wa nyumba za askari za Kikombo Dodoma kwa kuwa mafundi wamelipwa fedha zaidi ya gharama za kwenye mikataba na ulikuwa ujanja ili kuiba fedha za umma.

“Tulisema mjenge kwa force account ili kuwe na unafuu, lakini mnasema mmekwenda kununua Dar es Salaam wakati ndio bei zinazopatikana hapa Dodoma. Huo ulikuwa ni ujanja ujanja, Waziri muendelee kusimamia fedha za serikali maana fedha hizi ni za wananchi,” alisema Majaliwa na kuongeza:

“Sitegemei kuona suala hili likijirudia baada ya serikali kutoa fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa nyumba hizo.

“Kamishna, simamia kwa karibu ukamilishaji wa nyumba hizo huku ukihakikisha taratibu za manunuzi zinazingatiwa na pia kila kinachofanywa kiandaliwe taarifa.”

Alisema serikali haitasita kuwachukulia hatua za kisheria wote watakaobainika kuhujumu fedha za miradi ya maendeleo inayotekelezwa hapa nchini.

Majaliwa alisema serikali imetenga Sh bilioni 9.93 katika bajeti ya mwaka 2023/24 kwa ajili ya kukamilisha miradi ya ujenzi wa vituo saba vya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.

Vituo hivyo vitajengwa katika mikoa ya Songwe, Simiyu, Kagera, Njombe, Manyara, Katavi na Geita na kwenda sambamba na upatikanaji wa vitendea kazi vya kutosha vitasaidia kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao unakuwepo.

 

Habari Zifananazo

Back to top button