WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewashukuru wanamichezo na wasanii kwa mchango walioonesha katika kampeni za kuhamasisha jamii umuhimu wa kushiriki sensa Agosti 23, mwaka huu.
Akizungumza Dar es Salaam jana kwenye mkutano wa Kamati Kuu ya Sensa, Majaliwa alisema wote wamefanya kazi kubwa na kuwaomba kuendelea kuhamasisha jamii hadi mwisho.
“Niwashukuru wasanii mbalimbali waliohamasisha suala la sensa, wapo waliotunga nyimbo, kuandaa maigizo mafupi, waliochonga vinyago na kuweka kwenye mitandao yao ya kijamii, kwetu sisi ninyi ni watu muhimu,” alisema.
Alisema amefurahi kuona namna wanamichezo pia walivyohamasisha kwa namna tofauti kila mmoja na wengine kupitia matamasha akitolea mfano Wiki ya Mwananchi iliyoandaliwa na Yanga, Simba Day ya Simba, Azamka ya Azam FC na nyingine.
“Tumeona pia siku ya mechi ya watani wa jadi Simba na Yanga michezo ilivyohamasisha, yaliyotokea mengine sitayataja manake wapo watakaofurahi na wengine wataumia,” alisema.
Pia aliwashukuru wanamichezo waliokwenda kwenye michezo ya Jumuiya ya Madola Uingereza kuhamasisha sensa. Majaliwa alisema pia, katika Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) uliofanyika Arusha, aliona namna Shirikisho la soka nchini, TFF lilivyoweka hamasa mbalimbali.