WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa maagizo 12 kwa wafugaji na viongozi wa wizara kadhaa ili kumaliza migogoro ya wafugaji na wakulima hapa nchini.
Majaliwa alitoa maagizo hayo jana wakati wa mkutano wa siku mbili wa wadau wa sekta ya mifugo ukiwa na lengo la kuweka mwelekeo mpya wa sekta ya mifugo nchini.
Alisema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ana mapenzi ya dhati na sekta ya mifugo na anatamani kuona inaleta mapinduzi ya kiuchumi kwa kukuza zaidi pato la wananchi, kutoa ajira na kuchangia pato la taifa bila kuathiri mazingira na maendeleo ya sekta nyingine.
Kutokana na dhamira hiyo ya Rais Samia, Majaliwa alielekeza Wizara ya Mifugo na Mamlaka za Serikali za Mitaa kufanya tathmini ya maeneo ya ufugaji yaliyopo katika maeneo yao na kiasi cha mifugo kinachoweza kufugwa na endapo mifugo itazidi uwezo wa eneo husika, wafugaji waelekezwe kuvuna mifugo yao.
“Wafugaji wahamasishwe kuvuna mifugo yao kwa wakati ili kuwawezesha kupata bei nzuri sokoni pamoja na kupunguza changamoto za malisho hususani wakati wa ukame. Kwa ujumla kasi ya uvunaji wa mifugo nchini bado ipo chini ya asilimia 10 ikilinganishwa na viwango bora vya uvunaji wa mifugo kitaifa ambavyo ni kati ya asilimia 20 na 25,” alisema.
Pia Majaliwa alielekeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mamlaka za Serikali za Mitaa zihakikishe zinashirikiana na wadau wa sekta ya mifugo katika kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji na kutenga maeneo ya malisho ya pamoja, ranchi za vijiji na vitalu kwa ajili ya wafugaji binafsi.
Alisema kwa vijiji vyenye ardhi ya kutosha, vitenge maeneo ya ranchi za vijiji zenye ukubwa wa kati ya hekta 200 na 500 ambazo zitatumika kwa utaratibu wa kuwapanga wafugaji kutoka ndani ya kijiji husika. Majaliwa pia aliielekeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambayo inamiliki Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) ihakikishe maeneo yote ya NARCO yaliyoko kwenye mikoa yanabainisha umiliki.
“Wakuu wa mikoa kwanza nendeni mkatambue maeneo hayo yanamilikiwa na nani na mjue yapo katika wilaya gani na yana ukubwa upi na je, matumizi ni sahihi kama serikali inaotaka,” alisema na kuongeza: “Kwa sababu tuna watu binafsi wamechukua ardhi hiyo kazi yao ni kukodisha watu wengine, tumewaacha wafugaji wenye ng’ombe na tunawajua huyu ana ng’ombe wake 200, huyu ana ng’ombe wake 300 na tuna eneo la Narco zuri tu badala ya kumpa huyu mwenye ng’ombe tumempa mtu ambaye hana ng’ombe, halafu anakuja kumpangisha mwenye ng’ombe. Hii wakuu wa mikoa tuikatae wazi.”
Majaliwa pia aliagiza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na wadau na wafugaji kushiriki kikamilifu katika kuhamasisha mabadiliko ya mfumo wa ufugaji ikiwemo ufugaji wa kukaa katika eneo moja bila kuhamahama na wafugaji kulima malisho, badala ya kutegemea malisho ya asili peke yake.
Majaliwa aliagiza kuwa uzalishaji na usambazaji wa mbegu bora za mifugo uimarishwe ili kuongeza tija katika sekta ya mifugo na kuhamasisha wafugaji kutumia mifugo bora iliyofanyiwa utafiti na kuonesha kuwa na tija zaidi.
Pia, aliagiza wizara husika kuimarisha huduma za ugani kwenye sekta ya mifugo kwa kuweka vigezo vya kupima utendaji kazi na kuwafuatilia wagani wote nchini ikiwa ni pamoja na kuhimiza matumizi ya Tehama, kuendelea kuwapatia vyombo vya usafiri na mafunzo rejea kuhusu teknolojia mpya za ufugaji wenye tija na wa kibiashara.
Pia aliagiza Wizara ya Mifugo na Uvuvi ishirikiane na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi katika kutatua migogoro baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.