Majaliwa atoa maagizo Saba TCAA
DAR ES SALAAM: WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ametoa maelekezo saba kwa Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) ikiwemo Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kufanya marejeo ya viwango vya mikopo vinavyotolewa kwa wanafunzi wa urubani na kutoa kipaumbele kwa wahitaji wa fani za masuala ya usafiri wa anga
Pia, ameiagiza TCAA kuimarisha mifumo ya udhibiti wa matumizi mabaya ya viwanja vya ndege na kuhakikisha haviwi uchochoro wa kupitisha bidhaa haramu.
Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo katika maadhimisho ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwa TCAA katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Katika maagizo hayo Majaliwa pia amewataka wadau wote wa usafiri wa anga nchini kuteketeza majukumu yao kwa kufuata sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbali mbali inayosimamia masuala ya usafiri wa anga Kitaifa, Kikanda na Kimataifa kwa ajili ya kuhakikisha usalama ni kipaumbele namba moja.
Maagizo mengine aliyotoa ni kwa watendaji wa Mamlaka kufanya kazi kwa weledi na ubunifu ili kumudu soko la ushindani katika utoaji huduma za anga.
“Jifunzeni kutoka Mataifa yaliyofanikiwa zaidi ili kuongeza viwango vyetu vya kutoa huduma.” Amesema Majaliwa.
Pia, ameiagiza TCAA ibuni na kuongeza vyanzo vipya vya mapato ya Aviation Training Fund ili kuongeza idadi ya marubani wanaopata ufadhili wa masomo.
Aidha, amewataka watanzania kuendelea kuviamini na kutumia vyuo vilivyopo nchini vinavyotoa mafunzo ya utaratibu wa masuala ya anga.
“Vyuo vyetu vina uwezo mkubwa na vinaaminika barani Afrika, vitumieni na mviamini.” Amesisitiza.
Amesema, serikali imesimika mitambo ya kuongoza ndege katika viwanja vya Kimataifa vya Amani Abeid Karume Zanzibar na Julius Nyerere Dar es Salaam kwa ajili ya kuhakikisha ndege zinaruka na kutua kwa usalama.
“Serikali imepanga kuhimarisha sekta ya anga kwa kuwezesha ununuzi wa rada nne za kuongoza ndege za Kiraia, rada hizo tayari zimefungwa kwenye viwanja vinne vya mikoa ya Dar es Salaam, Kilimanjaro, Mwanza na Songwe. ” Amesema Majaliwa