Majaliwa atoa maelekezo 4 uhaba wa maji Dar
Awasha moto mamlaka za Bonde, Dawasa
UHABA wa maji jijini Dar es Salam, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa maelekezo mapya manne kwa Mamlaka zinazosimamia rasilimali za maji ikiwemo Bonde la Wami Ruvu.
Akizungumza mara baada ya kupokea taarifa ya hali ya maji kwenye Mkoa wa Dar es Salaam leo Novemba 2, 2022 Majaliwa amesemea licha ya Bonde la Wami Ruvu kupewa fedha nyingi lakini hakuna kazi ya ulinzi iliyofanyika.
Aking’aka Majaliwa amesema “Mkurugenzi wa bonde la mto Ruvu upo hapa, (Mhandisi Elibariki Mmasi) nataka nikwambie kwamba hatujaona kazi ya ulinzi wowote wa mto ule na kama hali hii itaendelea jiji la Dar es Salaam halitakuwa na maji milele.
“Ni lazima bonde liulinde mto huu kuhakikisha hakuna uchepushaji unaosababisha kuathiri mtiririko wa maji Ruvu Juu na Chini tumeipa fedha nyingi mamlaka nimwambie hatujaona kazi ya ulinzi ya mto ule ambao unategemewa na wakazi wa Dar es Salaam, Mamalaka hii tunaipa fedha nyingi kulinda.” Amesisitiza na kuongeza
“Mto huu haupo Pwani peke yake ukirudi nyuma Morogoro mpaka Tanga maeneo ya Kilindi yanaingiza maji mto Ruvu, Iringa na njia njia zote huu mto unatoka Mbeya Ihefu, na wilaya zake za Mbarali, kote huko ni vyanzo vya maji ambavyo vinaingiza maji Ruvu.
“Ni lazima sasa Bonde kuhakikisha mnalinda mfereji huu mpaka kwenye mikoa hiyo na kushirikisha wakuu wa mikoa hiyo, kuhakikisha mto Ruvu unalindwa kwa gharama yoyote ile na kutengeneza maji yake ili yapite maeneo yote na kama kuna matumizi yoyote yawe na utaratibu.” Amesisitiza.
Aidha, Majaliwa amesema Dawasa ndiyo mamlaka ya kuhakikisha maji wakati wote yanapatikana tena kwa kuwa na ziada ili ziwe zinatumika katika wakati wa changamoto kama iliyopo hivi sasa.
“Mamlaka hii kupitia mapato yake ni lazima itenge fedha kwa ajili ya kuchimba visima zaidi, kuna visima 197 vilifanyiwa savey (upembuzi) Mtendaji Mkuu (Mhandisi Cyprian Luhemeja) vipo wapi?
Luhemeja: Vipo Scatted maeneo mbali mbali lakini vingine vimepotea
Majaliwa: Vimepotea? Vimepoteaje poteaje? Fedha nyingi zilitolewa kwa nini vipotee?
Majaliwa: DC Temeke hali ya maji ipoje?
Jokate: Kuna baadhi ya maeneo wanapata maji, lakini kuna maeneo mengine ikiwemo Tuangoma hakuna maji.
“Dawasa nataka leo hii tenki hili lipeleke maji Kigamboni yote mpaka Mbagala, Tuangoma na Temeke yote, Kinondoni, Ubungo, Sinza, na Ilala ili kupunguza tatizo la maji…Nasisitiza leo hii, hakuna kutoka hapa mpaka maji yapatikane maeneo hayo, nitarudi hapa kwa muda wangu bila taarifa, ole wenu nisiwakute.”Amesema Majaliwa.
Amesema mahitaji ya maji katika mkoa wa Dar Es Salaam ni lita milioni 540 kwa siku na uzalishaji maji kwa siku ni lita milioni 520 katika kipindi ambacho kiwango cha maji katika Mto Ruvu kinakuwa katika hali ya kawaida, hivyo kuwa na upungufu wa lita zaidi ya milioni 20.
“Katika kipindi hiki ambacho kiwango cha maji katika Mto Ruvu kimepungua uzalishaji wa maji nao umepungua na kufikia lita milioni 300 kwa siku, hivyo kusababisha upungufu wa lita milioni 240.
“Kwa sasa tukiingiza lita milioni 70 kutoka katika mradi huu wa visima vya Kigamboni tutakuwa na upungufu wa lita milioni 174, hivyo tutaupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji katika baadhi ya maeneo.”Amesema
Pia, amemuagiza Waziri wa Maji Jumaa Aweso kushirikisha sekta binafsi katika miradi ya maji na si kuitegemea serikali pekee.
“Waziri tusitegemee Serikali peke yetu kutekeleza miradi hii ya maji, tumieni sekta binafsi na zenyewe ziingie zifanye kazi. Wapo watu wana fedha wanaweza kujenga miradi ya maji, muhimu wananchi wapate maji.”Amesema
“Mheshimiwa Waziri, hamisha mitambo yako DCCA (Wakala wa Uchimbaji Visima na Mabwawa) wataalamu wako chuo cha maji, waamie eneo hili kwenye visima vilivyopitiwa na wataalamu na kubaini kuwa vina maji ili waanze kazi hiyo mara moja, tusije fika Desemba hatuna maji….; “Maana hatuwezi kuchimba maji leo na leoleo kupata maji kwa mfumo huu ambao unaitaji maji kuanzia milioni 70 mpaka 100, ni lazima tuwe na mradi huu kwa wiki mbili tatu mtambo upo hapa ndani imekaa kwenye pointi zote tatu kati ya 10.
Pia, Majaliwa amemuagiza Aweso kupeleka mitambo kwenye visima 197 vilivyofanyiwa uchambuzi toka mwaka 1997.
“Maeneo yale yanatambulika na Dawasa wanayajua peleka mitambo kwenye maeneo hayo, anza kuchimba mifereji ya kuleta maji kwenye tenki hili ili kuleta maji kwenye mifumo.”Amesema