Majaliwa atoa maelekezo suala la maboma

DODOMA; Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza kufanyika kwa tathimini ya kubaini maboma yote ambayo hayajakamilika, kisha halmashauri iweke kwenye bajeti zao ili kukamilisha ujenzi uliokusudiwa.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum,Hawa Subira Mwaifunga wakati wa maswali kwa Waziri Mkuu, aliyehoji mkakati wa serikali kubainisha majengo yote ambayo ni maboma ili yamaliziwe na wananchi waone thamani ya nguvu yao, lakini pia waone thamani ya fedha za serikali zinazokwenda kwenye maeneo yao, ili yaweze kutumiwa.
Akijibu swali hilo Waziri Mkuu amesema suala la ujenzi wa miradi iwe ya elimu au afya ni jambo ambalo serikali imelielekeza kwenye serikali za mitaa.
“Tuna upatikanaji wa vyanzo aina mbili serikali kuu, kutoka serikali kuu tunapeleka fedha kwenye halmashauri za kujenga majengo hayo kwa thamani ya jengo lenyewe, kwa hiyo basi tunatakiwa kuwa na usimamizi baada ya kupokea fedha hizo ili kuona kwamba jengo husika linajengwa kwa thamani halisi ambayo wao walitoa makadirio na sisi tulepeka fedha.
“Lakini pia fedha aina ya pili ni ile ya itokanayo na mapato ya vyanzo vya ndani vya halmashauri ambapo hupanga mabeti kutokana na mipango yao,Maboma mengi yanatokana na mipango ya fedha hizo za halmashauri .
“ Niagize Tamisemi kwanza iendelee na utaratibu wa kubaini maboma yote yaliyojengwa na hayajakamilika.

Na wahakikishe wanaendelea kutenga bajeti za kuyakamilisha kwa sababu yametokana na mipango yao.

“Uzoefu tuliopata kutokana na ukaguzi wa miradi hiyo, majengo yote yaliyopelekewa fedha za serikali kuu yamekwenda kama yalivyopangwa na pale ambapo hayakukamilika hatua kali zimechukuliwa.
“Na wao wametakiwa kukamilisha fedha kwa sababu wameshindwa kukamilisha ujenzi wa majengo hayo kwa fedha iliyopelekwa, sasa kwa kuwa majengo mengi yanatokana na wao kushindwa kukamilisha bado wanatakiwa kuweka bajeti,” amesema.
Amesema mpango wa serikali ni kuhakikisha maboma yanakamilika kwa serikali za mitaa kufanya tathmini kwa miradi yake ione maeneo gani walianza miradi na kushindwa kuikamilisha na yamebaki maboma, ili wapange bajeti na kuikamilisha.

Habari Zifananazo

Back to top button