WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema Wizara ya Maliasili na Utalii imeunda kamati maalum kuhusu suala la uvamizi wa wanyama kwenye makazi ya watu na kwamba kama ripoti ya kamati hiyo itagusa sheria basi wizara itatoa muongozo wa nini cha kufanya.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo bungeni leo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Mwanga, Joseph Tadayo wakati wa maswali kwa Waziri Mkuu, ambapo Mbunge huyo alitaka kufahamu mikakati ya serikali kuhakikisha inapitia upya sheria za kulinda hifadhi ili pia zilinde wananchi na ikibidi kujitoa kwenye baadhi ya mikataba ya kimataifa ambayo sheria zake zina athari kwa wananchi na mali zao.
Katika majibu yake Waziri Mkuu amesema yamekuwepo malalamiko kuhusu wanyama kuharibu mali na hata kusababisha vifo katika baadhi ya maeneo.
“Wizara ya Maliasili imekuwa ikifanya taratibu kadhaa kukutana na taasisi zinazohusika kwenye uhifadhi wa mazingira yetu na hifadhi za wanyama wetu kuona wanyama wanabaki hifadhini na baadhi ya jitihada zilizochukuliwa ni kuongeza idadi ya askari walioweka vituo kandokando ya hifadhi hizo kuzuia wanyama wasiingie kwenye makazi ya wananchi, lakini pia jitihada za kufukuza wanyama kwa kutumia ndege kuwarudisha hifadhini.
” Tunajua ziko sheria zinalinda haya na mbunge ametaka tubadilishe sheria, lakini muhimu sasa tunataka wizara ihakikishe kuwa maeneo yote yaliyohifadhiwa kwa ajili ya kuweka wanyama yanaendelea kusimamiwa na sheria na taratibu ambazo mmezipanga kwa ajili ya kudhibiti wanyama hao kuingia kwenye makazi,” amesema.
“Ushauri wake kwa serikali tumeuchukua ila kwa vile tumeona wizara imeshaunda kamati tuiache ilete matokeo yake, lakini yote ni kama yatagusa kwenye sheria basi wizara itatuongoza katika kuleta sheria hapa tufanye mabadiliko ili tuweze kuhifadhi.
Lakini tuhakikishe kwamba wananchi wanaendesha shughuli zao na maisha yao yanaimarishwa na kulindwa kama ambavyo sheria hizi awali zilivyofanya na hatukuwa na tatizo hili, nikuhakikishie tunalinda maisha ya watu na wanyama hii ndio njia sahihi ya kuzuia madhara yanayojitokeza kwenye makazi ya watu,” amesema Waziri Mkuu.
–
Comments are closed.